Kagera. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amefika katika katika hospitali teule ya Biharamulo na kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya basi iliyotokea katika eneo la Kabukome, Kata ya Nyarubango wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
Ajali hiyo ilitokea jana Jumamosi Desemba 21, 2024 na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 16 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Capco One kufeli breki na kuserereka kinyumenyume kisha kugonga gari dogo.
Basi hilo liliokuwa linafanya safari kutoka Kigoma kwenda Bukoba wakati liliposimama kushusha abiria ambae alipitilizwa kwenye kituo, lilishindwa kuondoka na kuanza kurudi nyuma kisha kuacha njia na kupinduka.
Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi, Waziri Bashungwa ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na ajali hiyo na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwaombea majeruhi wapone haraka.
“Nitumie nafasi hii kuombea roho za marehemu ambao tumewapoteza katika ajali ambayo imetokea hapa Biharamulo, tumepoteza ndugu zetu 11, wametangulia mbele za haki,” amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara imeanza kufanyia kazi Maelekezo ya Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kufanya marekebisho ya kuwa na mfumo wa leseni za udereva ili kuwapunguzia alama madereva wanafanya makosa yenye kuhatarisha usalama barabarani ambazo zitapelekea kuwafungia leseni.
Kwa Upande wake, Mganga mkuu wa Hospitali teule ya Biharamulo, Gresmus Sebuyoya ameeleza kwa majeruhi 26 wameruhusiwa na wengine 16 wanaendelea na matibabu na ungalizi wa karibu.
“Tumebaki na watoto wanne ambao wanaendelea vizuri, wanaume tunao sita. Vifo tulikuwa navyo 11, wanawake watano, wanaume wanne na watoto wawili,” ameeleza Dk Gresmus.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.