Bosi mpya Geita ataja vipaumbele

SIKU chache baada ya kuapishwa kuendelea kuiongoza Chama cha Soka cha Geita kwa muhula mwingine kama  Mwenyekiti, Salum Kulunge ameanika vipaumbele 10 vya kufanyia kazi huku namba moja ikiwa ni kuendeleza soka la vijana ili kuzalisha wachezaji wengi.

Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Geita, Domisian Butula na Kassim Nangale walishinda nafasi ya ujumbe wa Kamatiya Utendaji, huku Mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa akishindwa kupatikana baada ya wagombea wawili, Simon Shija na Ally Ismail kulingana kura (8), hivyo, uchaguzi utarudiwa ndani ya siku 60.

Kulunge alisema ushindani ulioonyeshwa katika uchaguzi huo umetuma ujumbe wa namna gani wanachama wa chama hicho wanahitaji maendeleo huku imani waliyompa ikimpa motisha ya kupambana kuleta maendeleo ya soka mkoani Geita.

“Nawashukuru wajumbe kwa kuniheshimisha kuendelea kukitumikia chama kwa msimu mwingine wa nne siyo jambo dogo. Tuna vipaumbele 10 lakini miongoni kikubwa na cha kwanza ni kuhakikisha tunaendeleza soka la vijana,” alisema Kulunge na kuongeza;

“Hii ni sehemu ambayo nitaiwekea mkazo mkubwa sana na nimeeleza ninavyotaka kuanzia ligi ya mkoa wachezaji watakaokuwa na zaidi ya miaka 20 wasizidi watano, hili tutalisimamia na kamati zangu.”

Mtendaji Mkuu wa zamani wa Geita Gold, Simon Shija aliyegombea ujumbe wa mkutano mkuu taifa, aliwaomba wadau, wanamichezo, na makampuni mbalimbali mkoani humo kuunga mkono uongozi mpya wa Gerefa kwa kuwekeza katika soka la vijana na wanawake.

Shija ambaye pia ni Mwenyekiti chama cha soka wilaya ya Nyang’wale, alisema ndani ya miaka nane ya Kulunge tangu mkoa wa Geita uanzishwe amepiga hatua kubwa na matamanio ya chama hicho ni kuona anafanikisha mambo makubwa aliyoyaanzisha ikiwemo kukuza soka la vijana.

“Ndani ya miaka hii nane ameifanya Geita kuwa juu, sasa sisi wadau wa mkoa, wanamichezo, viongozi wa Serikali na makampuni tunawaomba waingie katika kudhamini mashindano mbalimbali ya soka la vijana na soka la wanawake,” alisema Shija.

Related Posts