Fadlu wala hana haraka | Mwanaspoti

SIMBA jana jioni imepata ushindi wa mabao 5-2 ugenini dhidi ya Kagera Sugar, huku Ellie Mpanzu akianza kwa mara ya kwanza, lakini mashabiki wa timu hiyo wanaona kama bado kikosi hicho kina haja ya kushusha mashine nyingine mpya ili utamu uzidi kukolea zaidi.

Hata hivyo kwa kocha wa timu hiyo, Fadlu David hesabu zake zipo kivingine kabisa akiamini hana sababu ya kuwa na papara ya kuleta majembe mengine kwa sasa kwani, kila kitu anakiona kinaenda sawa, lakini akitoa msimamo ambao ukisikiwa na mashabiki wa Simba watamuelewa.

Kocha huyo amesema kwa sasa hana haraka ya kuleta majembe na kutoa sababu ya uamuzi huo, huku akiwatuliza mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kula mtori nyama watakutana nazo chini.

Fadlu jioni ya leo alikuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini BUkoba kuiongoza Simba dhidi ya Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara na kushinda mabao 5-2, ameweka wazi msimamo wake katika dirisha dogo la usajili akisema hauwezi kumpiga tafu ili utafanyika kwa lengo la kuweka mambo sawa tu kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema anafahamu kiu ya mashabiki wa timu hiyo wakitaka kuona mastaa wakubwa wanashushwa, lakini kwa mtazamo wake bado Simba inahitaji madirisha mawili hadi matatu kuunda kikosi hatari kitakachotungisha zaidi Afrika.

Fadlu alisema usajili wa dirisha kubwa uliopita ulikwenda kutengeneza msingi wa kikosi hicho, ili kirudishe ubora wa kushindania mataji ambapo kazi hiyo bado unaendelea.

Alisema baada ya usajili huo wataongeza wachezaji wachache katika kila madirisha yanayofuata wakianza na dirisha hili dogo lililofunguliwa Desemba 15 na litakalofungwa katikati ya mwezi ujao mwakani.

Simba dirisha hili dogo staa wa kwanza watakayemuongeza ni winga Mpanzu aliyetarajiwa kuanza kutumika katika mechi ya jana akichukua nafasi ya mmoja wa makipa wa timu hiyo, Ayoub Lakred anayedaiwa ameachwa.

“Bado tuna kazi kubwa ya kutengeneza kikosi chenye ubora ambao tunataka au kile ambacho mashabiki wetu wanakitarajia,kujenga siku zote ni hatua endelevu sio kitu cha mara moja,”alisema Fadlu.

“Tulitumia dirisha lililopita kurudisha kikosi cha ushindani na naamini kila kitu kinakwenda sawa lakini bado hatujamaliza tutaendelea kufanya maboresho zaidi kwenye madirisha ya usajili yanayofuata,” alisema Fadlu na akuongeza; “Dirisha hili tutamuongeza Mpanzu huku tukiangalia nani mwingine tutampata, unajua shida ya dirisha kama hili ni vigumu kupata wachezaji Bora zaidi ambao timu zao zitakubali kuwaachia. Tutahitaji madirisha mawili zaidi baada ya hili ili kuweza kufanya maamuzi sahihi zaidi ya kuunda kikosi ambacho kitafanya makubwa hapa Afrika.”

Related Posts