Gamondi kuibukia AS FAR ya Morocco

WAKATI kukiwa na ukimya juu ya dili la kocha wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi kutua Singida Black Stars, inadaiwa kuwa, kocha huyo raia wa Argentina, yuko mbioni kujiunga na klabu ya AS FAR ya Morocco kama Mkurugenzi wa Michezo.

Ingawa taarifa hizi bado hazijathibitishwa rasmi, vyanzo vya karibu na klabu hiyo vinadai kuwa pande zote mbili zipo katika hatua za mwisho za mazungumzo. 

Gamondi, ambaye ana uzoefu mkubwa katika soka barani Afrika, alikuwa pia akihusishwa na Singida BS ya Tanzania katika wiki za hivi karibuni.

Hata hivyo, inaonekana kuwa klabu ya AS FAR imetangulia katika mbio za kumnasa kocha huyo kwa nafasi ya kiutawala badala ya benchi la ufundi. 

Iwapo tetesi hizi zitathibitishwa, uteuzi huu utakuwa sehemu ya mpango wa kimkakati wa AS FAR kuimarisha miundombinu ya michezo na kuongeza ushindani wa klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Gamondi ameonekana kama mtu sahihi kwa nafasi hiyo kutokana na ujuzi wake wa kiufundi na uzoefu wake katika kuendesha programu za soka, haswa katika mazingira ya Afrika. 

Hata hivyo, mashabiki wa soka wanabaki kusubiri kuthibitishwa kwa taarifa hizi huku wengi wakijiuliza ikiwa Singida BS wameachwa kwenye mazungumzo au kama bado wapo kwenye mbio za kumnasa kocha huyo mahiri.

Gamondi anakumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa kuacha rekodi kibao za kibabe ikiwemo kuifikisha timu hiyo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita huku akiwaacha na mataji Gamondi amechukua mataji matatu ambayo ni Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kukifanya kikosi hicho kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao ya Jamii kwa msimu huu.

Related Posts