Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura amemuhamisha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Ramadhani Ng’anzi kutoka kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani Tanzania kwenda makao makuu ya upelelezi Dodoma, kuwa mkuu wa kitengo cha makosa ya maadili ya Jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 22, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, nafasi ya Ng’anzi inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), William Mkonda.
Mkonda anayechukua nafasi ya Ng’anzi alikuwa mkuu wa usalama barabarani Kanda Maalum Dar es Salaam.
“Pia amemuhamisha aliyekuwa mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Dodoma. Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Boniphace Mbao kutoka Dodoma kwenda kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalum Dar es Salaam,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, IGP Wambura amemuhamisha aliyekuwa mkuu wa elimu kwa umma kikosi cha usalama barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Michael Deleli kwenda makao makuu ya Polisi Dodoma, kuwa kaimu mkuu wa maadhimisho ya kitaifa.
“Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nassoro Sisiwaya aliyekuwa mkuu wa operesheni kikosi cha usalama barabarani Tanzania anakwenda kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro,” imeeleza taarifa hiyo.