KINDA la zamani la Yanga U-20 anayekipiga Wakiso Giants ya Uganda, Isack Emmanuel Mtengwa amesema kocha wa timu hiyo ana mchango mkubwa kukua kwenye karia yake.
Ikumbukwe nyota huyo yupo Wakiso kwa mkopo wa mwaka mmoja pamoja na beki wa kati Shaibu Mtita ambao wote wameanzimwa kutoka Yanga ya vijana.
Akizungumza na Nje ya Bongo, Mtengwa alisema kocha wa timu hiyo ana msaaada kwenye karia yake kwani ni miongoni mwa watu wanaompa ushauri na kumwongezea kitu anapopata nafasi ya kucheza.
Aliongeza miongoni mwa vitu anavyomshauri ni pamoja na kumwelekeza namna ya mabeki wa pembeni wa kisasa wanavyotakiwa kupanda na kushuka kurudi kukaba ili awe mlinzi bora.
“Kocha anachonishauri kuongeza bidii kila kukicha ili nizidi kuwa bora kufanya mazoezi binafsi kaniambia itasaidia kwa kiasi kikubwa kufika mbali zaidi ya hapa licha ya hapo pia anaona kiwango changu kinazidi kuongezeka siku hadi siku,” alisema Mtengwa.
Licha ya chama la nyota huyo kuwa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa, lakini Mtengwa amekuwa akianza kwani kwenye mechi tano za mwisho ametumika kwa dakika 269.