KOCHA wa Kagera Sugar, Melis Medo, amesema kipigo cha mabao 5-2 walichokipata kutoka kwa Simba, wikiendi iliyopita, ni funzo kubwa kwa timu yake.
Katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba timu hiyo ya Kagera ilikubali kichapo hicho cha aibu kilichowafanya waonekane dhaifu mbele ya mabingwa hao wa zamani.
Medo, ambaye alikabidhiwa mikoba ya Kagera akirithi kutoka kwa Paul Nkata, Oktoba alisema kipigo hicho ni cha kwanza kikubwa kwa timu yake na ni ishara kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuimarisha timu hiyo.
Alisema kuwa timu yake ilifanya makosa mengi uwanjani, na makosa hayo ndiyo yaliyozaa matokeo hayo mabaya. Alikiri kuwa dhidi ya timu kubwa kama Simba, ambayo ina ubora mkubwa na wachezaji wenye uzoefu, kufanya makosa mengi ni hatari, na kwamba ni lazima wachukue kipigo hicho kama somo la kujipanga upya.
“Ni mbaya kufanya makosa mengi hasa dhidi ya timu yenye ubora kama wa Simba. Hili linatakiwa kuwa funzo kwetu, tunahitaji kujitathmini na kuangalia ni wapi tumekosea,” alisema Medo na kuongeza; “Tunahitaji kurekebisha udhaifu wetu na kuhakikisha tunarejea kivingine katika mechi zijazo.”
Kipigo hicho kimeifanya Kagera Sugar kushuka hadi nafasi ya pili kutoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa na pointi 11 tu, juu ya KenGold pekee yenye pointi 6.