Nyakati za sikukuu huwa za furaha kwa familia nyingi, hasa watoto wanaojawa na shauku ya kusherehekea sikukuu kwa michezo na safari. Hata hivyo, ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto ili kuepuka hatari zinazoweza kujitokeza.
Leo ningependa kuzungumzia mbinu msingi za kuwalinda watoto na maeneo salama wanayoweza kutembelea ili kufurahia sikukuu zao bila hofu ya kupatwa na madhara.
Ni vema mzazi kumwangalia mtoto au wanao kwa karibu siku hiyo, tunaambiwa ni hatua ya msingi katika kuhakikisha usalama wao.
Lakini pia inasaidia kuepuka kuwaacha watoto peke yao, hasa katika maeneo yenye watu wengi kama masoko, maeneo ya burudani na hata kwenye kumbi za michezo.
Lakini pia tumo kwenye ulimwengu wa kidijitali, watoto wanapaswa kujua namba za simu za wazazi au walezi wao. Hii itawasaidia kama wametoka peke yao na wakapatwa na tatizo, wanaweza kupiga simu kwa haraka hata kwa kuomba msaada wa watu walio karibu yao kuwasaidia kupata mawasiliano na wazazi wao.
Lakini pia waelimisheni jinsi ya kutambua watu wasiowajua au maeneo hatarishi. Kwa sababu mazingira wanapocheza watoto yanaweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wao.
Hivyo wazazi hakikisha maeneo wanayotembelea yanatimiza vigezo, mfano vya ulinzi wa kutosha.
Lakini pia mzazi unaweza kuchagua eneo la wanao kwenda kuburudika kwa ajili ya michezo yaliyo na usimamizi wa karibu na wafanyakazi wenye uzoefu.
Angalia pia vifaa vya michezo kama vile vitembezi, mabembea, na kutelezea vimewekwa vyema na havina hitilafu zinazoweza kuwa hatari kwao.
Na ni vyema kuchagua maeneo yasiyo na magari au yenye njia maalumu za watembea kwa miguu. Watoto wanaposhiriki katika shughuli za sikukuu, ni muhimu kuwapangia muda wa kukaa kwenye hayo maeneo.
Hivyo mzazi unaweza kuwapangia ratiba inayoeleweka ili waweze kufahamu muda wa kurudi nyumbani. Lakini waelekeze maeneo wanayopaswa kwenda yasiwe hatarishi kwao.
Kwa wale watoto wadogo msiwaruhusu kutoka peke yao, bali waongozane na mtu mzima kwa ajili ya kuwatazama kwa karibu wasipatwe na madhara.
Kila mzazi anajua wakati wa sikukuu, watoto hujishughulisha sana, hilo linaweza kuwaweka katika hatari ya kupata majeraha au maradhi. Hivyo wazazi mnapaswa kuwekeza katika vifaa vya huduma za kwanza ambavyo ni rahisi kufikiwa.
Lakini kila mzazi anatambua kuwa sikukuu ni siku ya kula vizuri na watoto hupenda kula vyakula vizuri, hivyo, ili kuwaepushia na hatari ya kuugua matumbo, wanapaswa kuandaa chakula salama kwa watoto wao ili kuepuka magonjwa ya tumbo.
Lakini pia wanapaswa kuwaelekeze kunawa mikono kabla ya kula au baada ya kucheza.
Kwa leo nihitimishe kwa kusema; “Kuwalinda watoto nyakati za sikukuu ni jukumu la msingi la kila mzazi na mlezi.”
Mnapaswa kuchukua hatua za tahadhari, kuchagua maeneo salama na kuhakikisha mawasiliano ya mara kwa mara kama watakuwa wameenda kutembea maeneo mbalimbali.
Kwa kuwalinda, basi watoto wanaweza kusherehekea sikukuu hizi za mwisho wa mwaka tukianza na ya Krismasi, kwa furaha na usalama. Hii si tu inalinda maisha yao, bali pia inawawezesha kufurahia wakati wao wa utoto bila hofu ya hatari.