Tunaishi katika nyakati ambazo maarifa kuhusu malezi ya watoto yamepata kipaumbele kikubwa, tofauti na miaka ya nyuma.
Pamoja na kuongezeka kwa mijadala kuhusu malezi kwenye majukwaa mbalimbali, suala hili limelenga zaidi hisia za watafiti kuliko ilivyokuwa zamani.
Kila siku, tafiti mpya zinaendelea kuchapishwa zikichunguza changamoto zinazoyakumba malezi ya watoto.
Hali hii inaweza kuleta wasiwasi kwa mtu anayefuatilia kwa makini. Anaweza kuuliza maswali kama, “Kwa nini kumekuwa na msisitizo huu mkubwa kuhusu malezi?” “Mbona wazazi wetu hawakupata elimu ya malezi lakini walifanikiwa kutulea vizuri?”
“Kwa nini licha ya kuwepo kwa maarifa mengi ya kisasa ya malezi, tunaendelea kuona kuporomoka kwa maadili kwa watoto wetu?” Maswali haya ni muhimu na yanahitaji majibu ya kina.
Hata hivyo, jambo la wazi ni kwamba jamii yetu inakutana na mabadiliko makubwa ya kijamii yanayoathiri mifumo ya malezi ya jadi. Ni muhimu kutazama mabadiliko haya na kuelewa jinsi yanavyohitaji marekebisho katika mbinu za malezi.
Mtindo wa maisha tunayoishi hivi leo unaathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyolea watoto wetu. Kwa mfano, siku hizi ni jambo la kawaida kwa wazazi kutumia muda mrefu mbali na familia zao. Kazi zinachukua muda mrefu wa wazazi kuliko ilivyopata kuwa hapo zamani.
Wakati zamani katika familia nyingi za kawaida baba na mama waliishi sehemu moja, siku za leo ni kawaida, kwa mfano, kusikia mume anaishi Dodoma, wakati mama anafanya kazi mkoani Arusha.
Katika mazingira haya, wazazi hawa wanaweza kukutana kwa nadra na hata kuchukua miezi kadhaa kabla mzazi mmoja hajapata muda wa kwenda kusalimia familia yake inayoishi mbali nae. Jambo hili halikuwahi kuwa sehemu ya maisha ya familia katika siku za nyuma. Kadhalika, ndoa nazo zimekuwa na mitikisiko kuliko ilivyokuwa zamani. Misukosuko ya ndoa inafanya watoto ama waishi na mzazi mmoja au wazazi wawili wasioelewana.
Siku za nyuma mama alikuwa ndiye mlezi mkuu. Katika familia nyingi za kawaida, wanawake walioolewa waliitwa ‘mama wa nyumbani.’ Kazi yao kubwa ilikuwa kubaki nyumbani muda mwingi kulea watoto. Wanawake wengi, kwa kawaida, hawakuwa na kazi nyingine zaidi ya kuwatunza watoto.
Kazi ya kutafuta kipato iliachwa kwa wanaume. Watoto walilelewa kwa karibu sana na mama tangu wakiwa wadogo mpaka walipofikia umri wa kuondoka nyumbani na kujitegemea. Hapakuwa na changamoto ya nani abaki nyumbani kuwaangalia watoto.
Mambo yamebadilika hii leo. Akina mama wameondoka nyumbani kuungana na wanaume kuongeza kipato cha familia. Dhana kuwa mwanamke ni ‘mama wa nyumbani’ inafutika. Akina mama wanafanya ujasiriamali, wanajihusisha na shughuli ambazo hapo zamani zilionekana kama haki ya wanaume.
Mwanamke kufanya kazi, kwa hakika si jambo baya. Jitihada za kuwasomesha watoto wa kike zinaenda sambamba na fursa ya kiajira sawa na mwanamume. Ndio kusema, kama mwanamume anaweza kuajiriwa, haileti maana kufikiri kuwa mwanamke anapaswa kubaki nyumbani kufanya kazi za ndani kama ilivyokuwa imezoeleka hapo zamani.
Katika ajira wanawake wameonesha uwezo wa kumudu majukumu yao sawa na wanaume. Karibu kila sekta hivi sasa wapo akina mama. Wanawake wanaonesha uwezo mkubwa. Wanashika madaraka makubwa makazini na wanafanya vyema, tena mara nyingine, kuliko wanaume.
Hata hivyo, mafanikio haya ya akina mama kikazi yametikisa maeneo mengineyo ya kijamii. Malezi ni eneo moja wapo kubwa lililokumbwa na tetemeko kubwa tangu akina mama walipoanza kuondoka nyumbani kuelekea makazini.
Kufifia kwa familia tandaa
Katika baadhi ya makabila, mwanamke ndiye aliyekuwa na jukumu la kuitunza familia. Ingawa mwanamke hakuwa na ajira rasmi, bado alitarajiwa kujituma katika shughuli zinazoingiza kipato cha familia. Mwanamke alishinda shambani akilima na pia alitafuta soko la mazao ya kilimo ili aweze kuilisha familia.
Hata hivyo, shughuli hizi za mwanamke hazikuathiri wajibu wake mkuu wa malezi. Kulikuwa na familia tandaa, ndugu wa ukoo, waliomsaidia kufanya majukumu ya nyumbani wakati yeye akiendelea na shughuli zake nyingine mbali na nyumbani.
Wakati mama akisafiri kwenda kuuza mazao mjini, kwa mfano, nyumbani walibaki ndugu waliomwangalia mtoto. Mama hakuwa na wasiwasi na usalama wa mtoto kwa sababu alijua amemwacha mtoto wa baba mkubwa, binamu au shangazi waliomjali mtoto wake kama ndugu.
Haya mawili, yalifanya suala la malezi kuwa jambo lisilo na changamoto kubwa. Kwamba baba akiwa kazini, mama alikuwepo nyumbani. Ikitokea mama naye anawajibika kufanya kazi nje na nyumbani, ilikuwepo familia tandaa kuhakikisha mtoto analelewa ipasavyo. Hata hivyo, ukaribu huu wa familia tandaa unaendelea kufifia. Kwa sababu kadhaa, imeanza kuwa nadra kuishi na watoto wa ndugu.