Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Mwanza kuongeza kasi ya usimamizi wa ujenzi wa daraja la Simiyu linaunganisha mkoa huo na Mara ili likamilike kwa wakati.
Daraja hilo lililoko wilayani Magu lina urefu wa mita 175 upana wa mita 12.3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita tatu, ujenzi wake ulianza Oktoba 30, 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili 29, 2025.
Akizungumza na wananchi waliofika kwenye daraja hilo jana jioni, Desemba 21, 2024, Waziri Mkuu alisema kukamilika kwa daraja hilo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Magu.
“Magu ni wilaya ya fursa kiuchumi, Magu ni pumulio la Jiji la Mwanza. Je, wanaMagu mmejipangaje kuzikamata hizo fursa? Ninawasihi jengeni vituo vya mabasi, mahoteli, maeneo ya vyakula na burudani,”alisema
Pia, Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao kujitahidi kuboresha miundombinu ya usafirishaji ili mtu akitoka Mwanza awe na uhakika wa kurudi kwa haraka bila shida yoyote.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa daraja hilo, Ofisa kutoka Tanroads makao Makuu, Katetula Kaswaga alisema mradi huo utakaogharimu Sh48 bilioni, unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.
“Mradi unajengwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) chini ya usimamizi wa mhandisi mshauri Tanroads Engineering Consulting Unit (TECU). Mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 35,” amesema.
Awali, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo, kutasaidia kupunguza ajali na msongamano kwa kiasi kikubwa kwani daraja la zamani lilikuwa na njia moja ila la sasa litakuwa na njia mbili.
Amesema ujenzi wa daraja la Simiyu ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini inayolenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
“Daraja hili lilijengwa kabla ya uhuru, lilikuwa limebakia peke yake kwenye barabara kuu za nchi nzima,” alisema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Sukuma katika Kata ya Ng’haya ambalo linaunganisha wilaya za Magu na Bariadi.
Daraja Sukuma lina urefu wa mita 70, upana wa mita 11.3 na barabara unganishi za kilomita 2.3, linajengwa na mkandarasi mzawa Mumangi Construction Co. Ltd.
Hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 24 na utagharimu Sh10 bilioni 10 hadi kukamilika kwake.
Akizungumzia mradi wa daraja la Sukuma, Kasekenya alisema ujenzi wa daraja hilo ni utekelezaji wa moja ya mikakati ya Serikali kuboresha sekta ya miundombinu nchini.
“Kukamilika kwa daraja hili kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa, pia kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda,”alisema.
Alisema daraja litakapokamilika na barabara hiyo ikaanza kutumika, itafupisha safari za kwenda mkoani Mara. “Barabara hii itakuwa fupi, ni kilomita 74 tu kwenda Mara,” alisema.