Mbowe ataka uchaguzi huru na haki Chadema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameziagiza mamlaka zinazosimamia uchaguzi wa chama hicho, kutenda haki ili ipatikane safu bora, yenye sifa na inayokubalika kuongoza.

Mbowe ametoa kauli hiyo ikiwa imepita wiki moja tangu katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika Desemba 16, mwaka huu kuwataka wagombea kuzingatia kanuni, katiba na miongozo ya uchaguzi, ikiwemo kutoshiriki vitendo vya rushwa.

“Niwatahadharishe katika kipindi cha kampeni niwaombe wagombea na wanachama kuzingatia, kanuni na katiba ya chama inayosimamia mchakato huu, ili tupate viongozi sahihi, kuna muongozo wa rushwa ni muhimu yote izingatiwe,” alisema Mnyika.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Desemba 22, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kurudisha fomu ya kuwania uenyekiti wa Chadema taifa, nafasi aliyohudumu kwa miaka 20.

Amesema anatamani kuona demokrasia ikitamalaki katika mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama hicho, kuwe na uwazi na kusiwepo dosari au doa.

“Naziagiza mamlaka za chama zinazohusika kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi huu zihakikishe uchaguzi wetu unafanyika vizuri na usiwe na doa, uwe wa uwazi, kila mtu aone, dunia ione, Chadema tunaweza kuchaguana bila kufanya wizi wa kura.

“Wizi wa kura si asili ya Chadema, ili yeyote atakayepatikana akawe halali si tu mbele ya wana Chadema, bali hata kwa Mungu,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, Mbowe amewahimiza walioingia kwenye kinyang’anyiro hicho kufanya kampeni za kistaarabu na zenye kukijenga chama hicho.

“Tusifanye kampeni za kuumizana kwa mambo ambayo si ya kweli, tukawe watu wa kweli wa kukilinda chama chetu, kulinda viongozi wetu na kulinda wanachama wetu, sisi ni familia kwani hauwezi kuharibiwa kwa sababu ya kutaka madaraka,” amesema Mbowe.

Kwa mujibu wa Mbowe, anatamani kampeni hizo zikakijenge chama hicho na kuonyesha kuwa na watu wastahimilivu kwa kuwa na viongozi wanaoweza kukutana na changamoto mbalimbali, lakini wakawa na kifua cha kutunza mambo.

“Natamani tukafanye kampeni zinazoweza kubadili na kukifanya Chadema kuwa bora katika malengo yetu ya kupigania haki, ya watu wake, uhuru wao na demokrasia ya watu wake na hatimaye maendeleo ya watu wote,” amesema.

Mshikamano katika kipindi cha kampeni ni jambo lingine lililosisitizwa na Mbowe, huku akitaka kila mmoja amjali mwenzake.

“Tunatambua kuna wanaotoka nje ya mstari katika kuendesha kampeni chafu, huo si utamaduni wa Chadema wala si utaratibu. Tunawaomba wale wote wenye nia ya kutugawa, basi wakapate busara ya kuacha tujenge chama chenye ustahimilivu, kabla na baada ya uchaguzi,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Mratibu wa Wanawake wanaomuunga mkono Mbowe, Rose Moshi amesema zaidi ya wanawake 400 walichanga na kufanikisha kulipia fomu hiyo kwa Sh1.5 milioni ikiwa ni kutekeleza ahadi yao.

“Hapa wanawake wengi wanatoka Kanda ya Pwani na baadhi kutoka kanda nyingine, wote kwa umuhimu wao waliona waache shughuli zao kuja kukuunga mkono kukusindikiza kurejesha fomu,” amesema.

Moshi amesema kitendo hicho ni ishara ya kuonyesha bado wanaimani atawavusha na kumtaka kiongozi huyo kuendelea kuwa na busara na hekima nyakati zote.

“Tunataka ukilinde chama hiki kwa wivu kubwa, kipekee kabisa uongozwe na hekima ili uweze kutuvusha katika nyakati nguvu tunazopitia na kuifanya nchi ipite salama,” amesema.

Moshi amesema wanamshukuru Mbowe kwa kuridhia ombi lao la kutetea nafasi hiyo, huku wakiahidi kumuombea.

Baada ya Mbowe kurejesha fomu, ni wazi sasa atakabiliana na upinzani kutoka kwa makamu mwa chama hicho bara, Tundu Lissu pamoja na Romanus Mapunda katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Januari 21, mwakani.

Related Posts