Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ama kipo uwanda wa kifo kisiasa au kinapitia agano la moto wa kukiimarisha.
Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara), Tundu Lissu, wamebeba haetima.
Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu 2020, anaungwa mkono na waumini wa falsafa ya “dawa ya moto ni moto”, huku Mbowe, anayekubalika kwa wanaomini “jicho kwa jicho huleta upofu”, wote wanautaka uenyekiti taifa.
Uchaguzi wa viongozi Chadema ngazi ya taifa, unaotarajiwa kufanyika Januari 2025, ndiyo utaamua chama hicho kitabaki katika hali gani. Kitadhoofika jumla kama NCCR-Mageuzi mwaka 1999 au itakuwa mwanzo wa Chadema mpya?
Uchunguzi ndani ya Chadema unaonyesha Mbowe, anaungwa mkono na viongozi wengi walioshinda uchaguzi ngazi za majimbo, mikoa na kanda, na hao ndiyo wanaendelea kuamini wimbo wa “Kamanda Tuvushe”, kwamba bila kiongozi huyo aliyeiongoza Chadema kwa miaka 20 sasa, chama hicho kitakufa.
Uchunguzi zaidi unatoa taswira kuwa viongozi wengi walioanguka kwenye uchaguzi wa majimbo, mikoa hadi kanda, wamejenga kinyongo kikubwa dhidi ya Mbowe, hivyo wanahitaji kupumua, endapo Lissu atafanikiwa kukalia kiti cha uenyekiti Chadema, watapumua na kupata matumaini mapya.
Desemba 12, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Lissu alitangaza hadharani nia ya kuwania uenyekiti wa Chadema taifa, aliulizwa swali kuhusu kuungwa mkono na waliopoteza uchaguzi, alijibu: “Kama hawa wanaoniunga mkono ni walioshindwa, basi nitaongozana na hawa losers (washindwa) wenzangu.”
Ndani ya Chadema, kuna sauti za wenye misimamo mikali, wanaoamini kwenye mapambano ya jino kwa jino, hao wamepata mwanga mpya kupitia Lissu, ambaye anafahamika kwa kuendesha siasa za makabiliano ya moja kwa moja bila kuzunguka. Wanaamini Lissu ataipeleka puta Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mnyukano wa Mbowe na Lissu umeshawishi wanaharakati wengi kujenga matamanio yao ndani ya kesho ya Chadema.
Wanaharakati waliojiweka wazi, wote wanamuunga mkono Lissu, hivyo kusababisha baadhi ya wanachama waandamizi wa Chadema kujitokeza kuwapinga.
“Hivi kwa akili ya kawaida, wana-Chadema tuwekewe mwenyekiti na akina Maria Sarungi (mwanaharakati) na Peter Msigwa (aliyeshindwa uchaguzi Chadema na kuhamia CCM).Kisha, kwa mihemko na mkumbo wa mitandao pamoja na makundi ya waliokosa uongozi Chadema wilayani, mikoani na kanda, tumwache Freeman Mbowe? Hiki ni chama cha siasa siyo NGO ya wanaharakati,” aliandika Yericko Nyerere, kada mwandamizi wa Chadema.
Timu inayomuunga mkono Lissu, inaamini Mbowe ameshafanya kazi kubwa kuifikisha Chadema mahali ilipo na amekwama, hivyo anahitaji kukaa pembeni ili chama kiongozwe na mtu atakayeweza kukifanya kiwe imara zaidi kukabiliana na dola.
Mdude Nyagali “Mdude Chadema”, kada mwandamizi wa Chadema katika moja ya mahojiano yake alisema: “Mbowe ni kama Musa, aliwatoa wana wa Israel Misri akawafikisha jangwani. Alihitajika Joshua awatoe Jangwani kwenda nchi ya Ahadi. Chadema ipo Jangwani, hapo ndipo Mbowe ametufikisha. Tunamhitaji Joshua. Lissu ndiye Joshua.”
Kwa mujibu wa tafsiri kuhusu maoni, mitazamo na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na mnyukano wa Mbowe na Lissu Chadema, wasiwasi mkubwa ni chama kugawanyika kuanzia ngazi ya uongozi hadi wanachama na wafuasi wa kawaida mitaani.
Endapo uchaguzi utafanyika, na kwa vyovyote vile ukaacha vinyongo kwa timu itakayoshindwa, unaweza kusababisha matokeo mabaya ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu 2025, kama ilivyotokea kwa NCCR-Mageuzi Uchaguzi Mkuu 2000.
Mnyukano mkubwa uliikumba NCCR-Mageuzi baina ya aliyekuwa mwenyekiti, Augustino Mrema dhidi ya Katibu Mkuu, Mabere Marando. Kutokana na kushindwa kuelewana, Mrema aliacha chama na kwenda kujiunga na TLP. Kisha, Marando alishindwa uenyekiti na James Mbatia.
Uchaguzi Mkuu 2000, NCCR-Mageuzi, ilianguka vibaya kutoka kuwa na wabunge 19 Uchaguzi Mkuu 1995 hadi mmoja. TLP ikanyanyuka, ikapata wabunge watano Uchaguzi Mkuu 2000. Hofu kuwa Chadema inaweza kurejea historia ya NCCR-Mageuzi inatokana na nguvu ya ushawishi waliyonayo Mbowe na Lissu.
Mfano kuhusu NCCR-Mageuzi, unahusika pia kwa Chama cha Wananchi (CIF), ambacho kilikuwa imara kwa miongo mitatu, lakini mwaka 2019 kilishuhudiwa kikipukutika baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kuondoka na kuhamia ACT-Wazalendo. Waliokuwa wabunge na viongozi karibu wote waliambatana na Maalim Seif.
Tathmini ndani ya Chadema inaonyesha kuwa Mbowe anakubalika kwenye mifumo ya chama hicho kuanzia ngazi za chini hadi wanachama. Hata hivyo, Lissu ana nguvu kubwa, sauti zinazomuunga mkono zinaonyesha kuwa ana ushawishi kwa wapigakura wengi, hivyo anaweza kuifanya Chadema ipate au ikose kura nyingi kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.
Lissu, alishakuwa mwanachama na aligombea ubunge kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi katika Uchaguzi Mkuu 1995. Baadaye alijiunga na Chadema, kipindi ambacho gari lilikuwa limewaka. Lissu akawa mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema, akiwa kwenye kundi lililofanikiwa kukifanya chama hicho kuongoza Kambi ya Upinzani Bungeni kwa mara mara ya kwanza mwaka 2010.
Kabla ya Lissu kuwa mbunge, Chadema ilikuwa imeshapitia majaribio mawili makubwa. La kwanza ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara), Chacha Wangwe kukusudia kumng’oa Mbowe kwenye uenyekiti. Kipindi hicho Mbowe alikuwa na muhula mmoja ofisini. Wangwe alifariki dunia kwa ajali kabla ya uchaguzi.
Jaribio la pili ni la Zitto Kabwe, aliyekuwa Naibu Katibu Chadema (Tanzania Bara), alitangaza kuwania uenyekiti dhidi ya Mbowe. Ni kipindi ambacho Zitto alikuwa kijana maarufu na mbunge mwenye ushawishi mkubwa. Wazee wa chama chini ya mwasisi, Edwin Mtei walimweka chini Zitto ambaye alikubali kujitoa kwenye kinyang’anyiro.
Zitto alikuwa mbele kwenye kinyang’anyiro, nyuma yake walikuwepo Profesa Kitila Mkumbo, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, David Kafulila, aliyepata kuwa Ofisa Habari wa Chadema, kada mwandamizi wa Chadema, Juju Danda, kutaja wachache.
Chadema walivuka salama mwaka 2009. Mbowe alishinda uenyekiti, akamteua Zitto kuwa Naibu Katibu Mkuu. Hata hivyo, Kafulila na Danda hawakubaki salama. Walivuliwa uanachama. Wakatimkia NCCR-Mageuzi.
Kitila alibaki, matokeo yake mwaka 2014 uligundulika waraka ambao maudhui yake yalikuwa kumshusha hadhi Mbowe kwamba hakuwa na uwezo wa kuongoza chama, vilevile kumkweza Zitto kuwa ni msomi na mwenye maarifa makubwa ya kiuongozi.
Ilibainika kuwa waraka huo waandishi wake walikuwa Profesa Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba pamoja na mtu mwingine ambaye hajawahi kutajwa. Hii inaonyesha kuwa Kitila alibaki Chadema, lakini dhamira yake ya kuona Mbowe anaachia madaraka ilikuwa palepale.
Waraka huo ni sababu ya Profesa Kitila, Mwigamba na Zitto kuvuliwa uanachama wa Chadema mwaka 2014 na 2015. Kilikuwa kipimo kwamba Chadema baada ya uchaguzi wa chama mwaka 2009, kiliishi ndani ya mgawanyiko kwa miaka zaidi ya mitano.
Kutoka mwaka 2015, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alipojivua uanachama wa chama hicho, baada ya kugomea ukaribisho wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyeteuliwa kuwa mgombea urais, hadi mwaka 2019, Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye alipojivua uanachama wa Chadema, vinyongo vimeendelea kutuama miongoni mwa viongozi, wanachama na wafuasi.
Kila hatua, mlaumiwa mkuu ni Mbowe. Mwaka 2009 hoja ilikuwa matumizi mabaya ya ruzuku na kukosekana uwazi kwenye mali za chama, mwaka 2024, agenda kuu ni kukaa madarakani muda mrefu. Mbowe alianza kupingwa akiwa na muhula mmoja tu ofisini.
Mwaka 2024, ni dhahiri Lissu amewaibua na wenye vinyongo vyao vya muda mrefu kuhusu Mbowe, sasa wanaungana na wanaharakati, wana-Chadema wenye misimamo mikali, vilevile walioanguka kwenye uchaguzi, kushughulika na Mbowe ili achomoke na kuruhusu mwanzo mpya wa Chadema.
Hoja ya Lissu kuhusu maridhiano ya chama hicho na CCM kuwa hayajawahi kuwa na faida yoyote, na majibu ya Mbowe kwamba faida zipo nyingi, vilevile kumkosoa Lissu kwa kukosa uadilifu wa vikao, inaonyesha chama hicho kipo hatarini. Zaidi, inaonyesha uamuzi wa vikao kwa wengine huona wanaburuzwa.
Kitendo cha Lissu kumtuhumu Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Ziwa, Ezekia Wenje kuwa alimpeleka nyumbani kwake mtu anayeitwa Abdul ili kumhonga, kisha Wenje kujibu kwamba alimpeleka Abdul kwa mwaliko wa Lissu ili asaidie kulipwa fedha za matibabu, kinatafsiri kutoaminiana na kusemeana uongo.
Kauli ya Wenje aliyonukuliwa akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni akisema kuwa Lissu alimwita yeye na viongozi wengine na kuwathibitishia kwamba Mbowe alihongwa magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser, wakati Mbowe aliyanunua mnadani, inatoa picha kuwa mgogoro wa Chadema umekuwa ukifukuta muda mrefu.
Hali halisi Chadema na jinsi moshi unavyofuka sasa ni matokeo ya moshi wa pumba. Unapoona moshi kwenye pumba, ujue ndani yake moto ni mkali. Chadema ni moto wa muda mrefu na sasa ni matokeo. Hakuna wakati Mbowe amewahi kupingwa hadharani kama sasa.