Kiongozi wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Syria aliyeko ziarani nchini humo amesema Jumapili kuwa kuna uwezekano wa kupata “ushahidi wa kutosha kabisa” wa kuwafungulia mashtaka watu waliotenda uhalifu dhidi ya sheria za kimataifa, lakini alisisitiza haja ya haraka ya kuuhifadhi na kuulinda ushahidi huo.
Milango ya magereza ya Syria ilifunguliwa baada ya muungano wa waasi unaoongozwa na kundi la Hayat Tahrir Al-Sham kumwondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad mwezi huu, zaidi ya miaka 13 baada ya ukandamizaji wake wa kikatili wa maandamano ya kupinga serikali kuzua vita vilivyoua zaidi ya watu 500,000.
Soma pia: Miaka 10 ya mauaji, mateso na wakimbizi Syria
Wakati familia zikikimbilia magereza ya zamani, vituo vya kizuizi, na makaburi ya halaiki yaliyoshukiwa, wengi wameonyesha wasiwasi kuhusu ulinzi wa nyaraka na ushahidi mwingine.
“Tuna uwezekano hapa wa kupata ushahidi wa kutosha uliosalia nyuma ili kuwafungulia mashtaka wale tunaopaswa kuwafungulia mashtaka,” alisema Robert Petit, kiongozi wa Mfumo wa Kimataifa wa Haki na Huru wa Umoja wa Mataifa (IIIM) ulioanzishwa mwaka 2016 kwa ajili ya kuandaa mashtaka kwa uhalifu mkubwa wa kimataifa uliofanyika Syria.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kuhifadhi ushahidi “kunahitaji uratibu mkubwa kati ya wadau mbalimbali.”
“Tunaweza kuelewa hisia za kibinadamu za kuingia na kujaribu kuwatafuta wapendwa wako,” alisema Petit.
“Hata hivyo, ukweli ni kwamba, kuna haja ya kuweka udhibiti ili kuzuia uingiaji kwenye vituo hivi vyote tofauti… Inahitajika juhudi ya pamoja ya kila mtu mwenye rasilimali na uwezo wa kufanya hivyo ili kulinda ushahidi.”
Soma pia: Aleppo yatendewa ukatili – UN
Shirika hilo, halikuruhusiwa kufanya kazi Syria chini ya serikali ya Assad lakini liliweza kuhifadhi ushahidi mwingi kutoka nje ya nchi.
Tangu kuondolewa kwa Assad, Petit ameweza kutembelea nchi hiyo lakini timu yake bado inahitaji idhini ya kuanza kazi yao ndani ya Syria, ombi ambalo tayari limetolewa.
Alisema timu yake imehifadhi kumbukumbu za “mamia ya vituo vya uzuwiaji… Kila kituo cha usalama, kila kambi ya kijeshi, kila gereza kilikuwa na kizuizi au makaburi ya halaiki yaliyohusiana nacho.”
“Sasa tumeanza kugusa juu tu ya tatizo hilo na nadhani itachukua muda mrefu kabla ya kujua ukubwa wake wote,” aliambia shirika la habari la AFP.
Shirika la uangalizi: Zaidi ya 100,000 waliuawa magerezani
Kulingana na shirika la uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria, zaidi ya watu 100,000 walifariki katika magereza na vituo vya vizuizi vya Syria tangu 2011.
Kituo cha Saydnaya, mahali palipotendeka mauaji ya kiholela, mateso na utoweshwaji wa nguvu, kilikuwa mfano wa ukatili uliofanywa dhidi ya wapinzani wa Assad.
Petit alilinganisha Saydnaya na gereza la S-21 katika mji mkuu wa Cambodia, Phnom Penh, ambalo lilijulikana kwa ukatili wa Khmer Rouge na sasa linahifadhi jumba la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari nchini humo.
Soma pia: Mauaji mengine ya maangamizi yahofiwa kufanyika Syria
Kituo cha Saydnaya kitakuwa “mfano maarufu wa ukatili wa kibinadamu,” alisema.
Petit alisema timu yake imewasiliana na mamlaka mpya “kuomba idhini ya kuja hapa na kuanza kujadili mfumo wa namna ya kutekeleza jukumu letu.”
“Tulikuwa na mkutano wenye mafanikio na tumeomba rasmi sasa, kulingana na maelekezo yao, kurudi na kuanza kazi. Kwa hivyo tunasubiri jibu hilo,” alisema.
Hata bila kufika Syria, timu ya watu 82 ya Petit imekusanya ushahidi mwingi kuhusu uvunjaji mbaya wa sheria za kimataifa uliofanyika wakati wa vita.
Lengo ni kwamba sasa inaweza kuwepo mchakato wa uwajibikaji wa kitaifa Syria na hatua zichukuliwe hatimaye kuipa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mamlaka ya kushughulikia uhalifu uliofanyika nchini humo.