BEKI mpya wa Namungo, Mrundi Derrick Mukombozi amesema amejisikia fahari kucheza tena mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara juzi dhidi ya JKT Tanzania, huku akiweka wazi ana kazi kubwa ya kufanya ili kucheza kikosi cha kwanza.
Nyota huyo amerejea tena ndani ya kikosi hicho katika dirisha hili dogo la usajili akiwa mchezaji huru baada ya kuondoka msimu uliopita, ambapo juzi aliingia akitokea benchi akichukua nafasi ya Lenny Kissu wakati timu hizo zilipotoka suluhu.
“Ni furaha kwangu kurejea tena na kuendelea kupata nafasi ya kucheza, natambua msimu uliopita na huu wa sasa haitokuwa rahisi kuingia kikosi cha kwanza moja kwa moja kutokana na ushindani hivyo, ni jukumu langu kupambana zaidi,” alisema.
Beki huyo aliyefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa na timu hiyo huku akiwa panga pangua, aliongeza uwepo wa mabeki wengine akiwemo, Daniel Amoah aliyewika na Azam FC, utaongeza chachu ya ushindani kikosini msimu huu.
“Ili siku zote uonekane bora ni lazima upambane na waliokuzidi au unaoendana nao, wapo mabeki wazuri ambao nimewakuta na wengine huenda wakaongezeka, ingawa kwangu ni jambo ninalofurahia kuona ushindani ukiwa ni mkubwa kwa manufaa ya timu.”
Kwa upande wa Kocha wa Namungo, Juma Mgunda alisema maboresho ya wachezaji katika dirisha hili ni mikakati ya kukisuka upya kikosi hicho kutokana na upungufu uliokuwepo, huku akiweka wazi wote waliosajiliwa hadi sasa ni bora na wazoefu.
Mbali na Mukombozi na Amoah, wengine waliosajiliwa na ‘Wauaji hao wa Kusini’ ni aliyekuwa beki wa kushoto wa timu hiyo, Emmanuel Charles aliyerejea kwa mara nyingine akitokea Kagera Sugar na kiungo, Najim Mussa kutokea Singida Black Stars.