Dodoma. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeeleza kuwa uwekezaji wao katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma wenye thamani ya Sh148.4 bilioni, ikiwemo ujenzi wa hoteli ya nyota tano, utarejesha gharama ndani ya kipindi cha miaka 11.
Mradi huo unajumuisha hoteli itakayokuwa na vyumba 120 pamoja na chumba maalumu cha hadhi ya urais, ofisi, maduka makubwa, sehemu ya mazoezi na benki.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba akizungumza jana Jumamosi, Desemba 21, 2024 katika hafla ya upandaji miti na utambulisho wa mradi wa uwekezaji eneo la Njedengwa, Dodoma amesema mradi huo umefanyiwa tathmini ya kina kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuutekeleza.
“Mradi huu utagharimu takribani Sh148.4 bilioni na utalipa ndani ya miaka 11. Ujenzi rasmi utaanza Mei, 2025, kwa sasa tunaendelea na taratibu za kumpata mkandarasi, hatua za awali zimeshaanza, na tathmini za mwisho zitakamilika Machi 2025 ili ujenzi uanze,” amesema Mshomba.
Amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Juni 14, 2023 mkoani Mwanza alipotembelea mradi wa hoteli ya NSSF katika eneo hilo.
Rais Samia aliagiza maeneo mengine ya uwekezaji yaainishwe, baada ya kufanyika tathmini ya kina kuona kama yatarejesha thamani ya uwekezaji huo.
Mshomba amesisitiza kuwa jukumu la msingi la NSSF ni kutunza fedha za wanachama kwa kuwekeza katika miradi yenye tija na usalama, ili kuhakikisha mapato yanayotokana na uwekezaji huo yanatumika kutimiza malengo ya msingi, ikiwemo kulipa mafao ya wanachama.
“Uwekezaji huu unahitaji umakini mkubwa, kwani kutokuwa makini kunaweza kusababisha kushindwa kutimiza wajibu wetu wa kulipa mafao. Tunahakikisha kila uwekezaji wetu unaongeza mapato na kuhakikisha usalama wa michango ya wanachama wetu,” amesema Mshomba.
Kwa upande wake, meneja miradi wa NSSF, Helmes Pantaleo amesema wameshapata mwendeshaji wa hoteli hiyo, Kampuni ya Ako Hospitality kutoka Dubai.
“Tumefanya tathmini ya mazingira, mkandarasi ndiye atakayechora na kujenga. Uchunguzi wa udongo, hali ya tetemeko, na uwepo wa mapango umeshafanyika, na ripoti ya mwisho tumepokea Novemba 20, 2024,” amesema Pantaleo.
Amesema makandarasi sita wameshapitishwa na Januari 2025 watapewa nyaraka husika, huku mchakato wa manunuzi ukitarajiwa kukamilika Machi 2025 na maandalizi ya awali yataanza Aprili na ujenzi utaanza rasmi Mei 2025.
Pantaleo amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miaka mitatu ya ujenzi (2028).
Jengo hilo litakuwa na ghorofa 16, litakuwa jengo refu zaidi mkoani Dodoma. “Dodoma watu wengi hawajengi maghorofa marefu kutokana na hofu ya tetemeko, lakini sisi tumefanya tathmini ya kutosha kuhakikisha uimara wa jengo hili,” amesema Pantaleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akizungumza katika hafla hiyo, ameipongeza NSSF kwa uwekezaji huo mkubwa unaotarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kufungua fursa kwa mikutano mikubwa kufanyika jijini Dodoma.
Sifa za hoteli ya nyota tano
Kwa mujibu wa viwango vya hoteli za nyota tano, hoteli hiyo itakuwa na:
- Vyumba vingi vya kulala pamoja na huduma za hali ya juu
- Maduka ya kubadilishia fedha na bidhaa muhimu
- Sehemu za chakula na vinywaji
- Mawakala wa mashirika ya ndege
- Kumbi kadhaa za mikutano
- Bwawa la kuogelea
- Huduma za kufua nguo.
- Mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti.