Power Mabula; Jitu la miraba minne lenye nguvu za ajabu

Power Mabula alitambulika kwa uwezo wake wa kuzuia gari aina ya Land Rover kwa maneno tu, kupitisha gari kifuani na kuhimili kuvunjiwa matofali kwa kifua kwake. 

Leo hii, Power Mabula ameokoka na anahubiri Injili kwa jina la Mchungaji Mwakaseka, akifanya huduma zake wilayani Kilindi, mkoani Tanga.

Tofauti na wanamichezo wa nguvu za mwili (ma-power) wa sasa ambao huonyesha uwezo wao kwa kunyanyua vitu vizito, kushiriki mieleka, na kuzuia magari au pikipiki, Mabula hakujihusisha na mieleka. 

Katika miaka ya 1970 hadi 1980, aliingia mitaani akitumia gari aina ya Land Rover 109, akijionyesha misuli yake kama njia ya kuhamasisha watu kuhudhuria maonesho yake. 

Power Mabula katika moja ya harakati zake

Hii ilikuwa tofauti na sasa ambapo matangazo hupambwa na picha za wahusika mitaani.

Power Mabula alikuwa ni mfano wa chuma, mrefu, mwenye nguvu na mwili wa mawe.

Uwezo wake ulijumuisha kulala juu ya misumari, kunyanyua vitu vizito, kuzuia pikipiki zaidi ya kumi zisisogee na kunywa juisi ya ‘orange squash’ yenye ujazo wa lita moja kwa kila chupa bila kuchanganya na maji. 

Juisi hii, iliyotengenezwa kwa machungwa halisi huko Tanga, ilikuwa na ladha safi na ilionekana kuwa moja ya alama za maonesho yake.

Maonesho yake yalivuma mikoani, hususan nyakati za sikukuu kama Eid, Pasaka, na Krismasi. 

Power Mabula alijizolea mashabiki wengi waliovutiwa na nguvu zake za ajabu. 

Hata hivyo, licha ya kuwa mahiri katika michezo ya kutumia nguvu, hakuwahi kushiriki mieleka kama ma-power wengine wengi waliokuja baadaye.

Power Mabula anavyoonakana kwa sasa akiwa mchungaji.

Katika mahojiano, Mabula aliwahi kueleza sababu za kudorora kwa mchezo wa “u-power”. 

Alisema vijana wa sasa wamekosa ujasiri wa kuingia kwenye mchezo huo. “Uoga umesababisha ukosefu wa wachezaji wapya. 

Vijana wa sasa wanauangalia mchezo huu kwa jicho tofauti. Wengi wanashughulikia kujaza miili yao ili kuwa mabaunsa au kutunisha misuli kwa sababu za kijamii, lakini hawajiingizi katika kuwa pawa wa kweli,” alisema Mabula.

Kwa sasa, Power Mabula amebadilisha mwelekeo wa maisha, akitumia historia yake ya kipekee kuwavuta watu kwa injili, huku akibaki kuwa mfano wa kujituma, uthubutu na kujitofautisha.

‘Ma-power’ wacheza mieleka

Katika historia ya maonesho ya nguvu za mwili nchini, kulikuwapo wanamichezo waliovutia umma kwa uwezo wao wa kushangaza. 

Miongoni mwao alikuwapo mwanamke pekee aliyejulikana kama Power Agnes. 

Power Agnes alijipambanua kwa uwezo wake wa kubeba kreti mbili za bia zikiwa na vinywaji kwa meno na kutembea nazo kwa dakika kadhaa kabla ya kuzishusha. 

Aidha, alikuwa na uwezo wa kuhimili kuvunjiwa matofali mawili mgongoni kwake na mtu mwenye nguvu kwa kutumia nyundo kubwa.

Enzi hizo, kulikuwapo pia na orodha ndefu ya ‘ma-power’ ambao walishiriki maonesho ya nguvu za mwili, wengine pia wakijihusisha na mieleka. 

Miongoni mwa majina yaliyotamba ni Power Bernadi, Power Chaka, Power Iranda (Chazi Mbwana), Power Nyati, Power Bukuku, Sumu ya Mamba, Shot Power ‘Danger Boy’, Power Vice Bironda, Power Benado, Power Mashaka, na Power Badru Nassoro. 

Wengine ni Power Jafar Vuru Mroma, TX Chaka, Power Mwanza, Power Singambele Safi, Power Mmasai na Power Nasoro Magazine.

Wakati wengine kati yao bado wako hai wakijivunia umri mkubwa, wengine wametangulia mbele ya haki. 

Kila mmoja alichangia kwa njia ya kipekee katika burudani na kuvutia maelfu ya mashabiki wa maonesho haya ya kipekee.

Katika mahojiano, Aloyce Melchiory, maarufu kama Power Mmasai, alikanusha dhana ya kuwapo kwa ushirikina kwenye mchezo huu. 

Alifafanua kwamba nguvu hizi ni matokeo ya mazoezi makali, nidhamu na matumizi ya akili.

“Hakuna ushirikina kwenye mchezo huu. Yote ni sayansi ya akili na mazoezi. Mfano, mtu anapitisha gari kifuani au kunyanyua vitu vizito kwa meno; hiyo ni sayansi tu ya mwili na akili,” alisema Power Mmasai. 

Aliongeza kuwa magari yanayopitishwa kifuani ni ya kawaida kama pick-up au Land Rover, ambayo uzito wake unalingana na uwezo wa mchezaji.

“Sijawahi kusikia ‘power’ anapitisha kifuani Scania, mara zote ni magari haya ya kawaida tu kama pick-up au Land Rover ambayo yanaendana na uzito wa mhusika, hivyo ukiondoa uoga na kujiamini, pia ukiwa umefanya mazoezi yote hayo yanawezekana.

 “Ndiyo sababu mchezo huu ukaitwa mchezo wa nguvu, unaponyanyua kreti kwa meno au tofali au hata kuzuia pikipiki kwa kifua, ile ni sayansi tu ya kawaida,” anasema Power Mmasai.

Kwa upande wake, Power Iranda alieleza tofauti kati ya ‘power’ na mazingaombwe. 

Anasema, mtu anaweza kuwa mwanamieleka pia akawa power, lakini michezo hiyo haiusiani na mazingaombwe

“Mazingaombwe ni hali ya kubadilisha kitu kimoja kuwa kingine, kama karatasi kuwa kitambaa. Lakini ‘power’ ni kutumia nguvu kutoa burudani na mtu anaweza pia kuwa mwanamieleka na bado akawa ‘power’,” alisema.

Related Posts