RAIS SAMIA AFUNGUA UCHUMI WA NCHI KWA KUKARIBISHA WAWEKEZAJI NCHINI-ULEGA

 

 

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani  Disemba 22,2024

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa kwa mwaka 2024, mitaji ya uwekezaji wa kimataifa iliyoingia nchini imeongezeka kwa asilimia 26, ikiwa ni jumla ya dola bilioni 42.1 za Kimarekani.

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha viongozi mbalimbali, wawekezaji, na wananchi katika stendi ya zamani ya Mailmoja, Kibaha, Mwishoni mwa wiki Ulega alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua uchumi wa nchi na kuvutia wawekezaji wa kimataifa.

Kutokana na ukuaji huo, Ulega alitoa rai kwa  wamiliki wa viwanda kutumia malighafi zinazozalishwa ndani ya nchi ili kulinda wawekezaji na kuimarisha ustawi wa soko la ndani, ambalo ni msingi wa ukuaji wa uwekezaji .

“Wenye viwanda wanapaswa kuchangamkia fursa ya kutumia malighafi zinazozalishwa nchini na kujivunia bidhaa za ndani kwani soko la mwanzo ni sisi wenyewe watanzania” alisema Ulega.

Hata hivyo alieleza ili kukabiliana na changamoto ya foleni ambazo zinadidimiza Uwekezaji na biashara Serikali inakwenda kufanyia kazi changamoto iliyopo Barabara Kuu ya Morogoro pamoja na ile Kilwa kutokea Rangi Tatu -Kongowe hadi Mwandege.

Ulega amemuelekeza ,Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS )Mkoani Pwani injinia Baraka Mwambage, kusimamia fedha za usanifu wa barabara kuanzia Mailmoja -Pichandege hadi Misugusugu kiasi cha sh. bilioni moja.

Alieleza, upande wa barabara inapoishia njia nane Kibaha Mailmoja hadi Pichandege kuna maelekezo ya kupanua barabara hiyo ambapo fedha ya usanifu ni bilioni moja ili kuutengeneza mji huo, kuingia kwenye maingilio ya Serikali na kwenye miji ya watu.

“Haya ni maelekezo mahsusi, nitahakikisha nayasimamia usiku na mchana maelekezo hayo kutoka kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambae amejipanga kuinua sekta ya viwanda na Uwekezaji nchini” alisisitiza Ulega.

Katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya utanuzi wa barabara ya Mbagala Rangi Tatu -Kongowe hadi Mwandege km 3.8 eneo korofi kazi inaenda kufanywa, Tunamshukuru Rais kuridhia fedha za fidia kiasi cha sh bilioni 12.6 sambamba na kujenga daraja la Mzinga.

Waziri huyo wa Ujenzi ,aliwataka wakandarasi kuachakufanya kazi kwa mazoea,kwani wamekuwa wakifanya kazi ama marekebisho mchana pekee na kusababisha kero kwa wananchi.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani,alhaj Abubakar Kunenge, alielezea hatua zinazochukuliwa kumaliza changamoto ya upungufu wa umeme kutokana na ongezeko la vyanzo vya nishati.

Kwa niaba ya wakuu wa wilaya mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir, aliomba serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya miundombinu, ikiwemo umeme, maji na barabara, ili kuwasaidia wawekezaji.

Mkurugenzi wa TCCIA, Oscar Kisanga, alibainisha sekta binafsi ni kiunganishi kati ya wafanyabiashara na Serikali.

Kisanga alihimiza,sekta binafsi kushiriki kikamilifu kupitia maonyesho ya viwanda na biashara kwa lengo la kutafuta masoko na kujitangaza.

 

Related Posts