Hanang. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Theresia Irafay, kumuondoa Mkuu wa Shule ya Sekondari Chifu Sarja, Eelifadhili Gefi, kutokana na kushindwa kuisimamia shule hiyo ipasavyo.
Sendiga ameonesha kutoridhishwa na utendaji wa mkuu huyo wa shule, hususan kutokuwepo mara kwa mara anapofanya ziara shuleni hapo. Agizo hilo limetolewa leo Jumapili, Desemba 22, 2024, baada ya Sendiga kufika shuleni hapo kwa mara ya pili mfululizo bila kumkuta mkuu huyo wa shule.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa amefanya ziara shuleni hapo zaidi ya mara mbili bila kukutana na mkuu wa shule hiyo, hali inayotia shaka uwajibikaji wake.
“Kama mkuu wa shule hayupo, atawezaje kuwasimamia walimu na kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa ufanisi? Nani anaweza kujibu maswali yangu ikiwa mkuu hayupo? Hivyo aondolewe na nafasi yake apewe mwalimu mwingine atakayetekeleza majukumu kwa ufanisi” amesema Sendiga.
Ziara ya Sendiga ililenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo iliyopo Kata ya Endasak, lakini kutokuwepo kwa mkuu wa shule kumeonekana kuwa kikwazo kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Aidha, Sendiga amesisitiza umuhimu wa viongozi wa taasisi za elimu kuwa mifano bora ya uwajibikaji na kuhakikisha wanahamasisha maendeleo katika maeneo yao.
Shule ya Sekondari Chifu Sarja inajenga baadhi ya majengo, inadaiwa ujenzi wake umeshindwa kukamilika kwa wakati bila sababu za msingi.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, Mwalimu Gefi, amesema yuko safari na ofisi yake amekaimisha kwa mwalimu mwingine ambaye hata hivyo, hakumtaja kisha akakata simu.
Kwa upande wake mkazi wa eneo hilo, John Anney amepongeza hatua ya mkuu wa mkoa, akisema kuwa mabadiliko hayo yataongeza kasi ya ujenzi wa shule hiyo.
“Ujenzi umekuwa wa kusuasua, lakini sasa tuna matumaini kuwa utamalizika kwa wakati,” amesema Anney.