Sababu Desemba kuwa na ajali nyingi zatajwa

Dar es Salaam. Mfululizo wa matukio ya ajali katika kipindi cha mwisho wa mwaka, umehusishwa na wingi wa vyombo vya usafiri barabarani, madereva wa magari binafsi kukosa uzoefu na barabara nyembamba.

Hayo yamesemwa wakati ambao, taarifa mbalimbali zinaonyesha katika kipindi cha wiki tatu, watu 35 wamepoteza maisha, huku 38 wakijeruhiwa kutokana na matukio ya ajali ndani ya Desemba, 2024.

Hata hivyo, wadau wa usafiri na wanazuoni wamehusisha wingi wa matukio hayo ya ajali ya mwisho huu wa mwaka na mabadiliko yaliyofanywa katika Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, wakisema ni kuonyesha uwajibikaji.

Katika taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa leo Jumapili Desemba 22, 2024, aliyekuwa Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani, Ramadhan Ng’anzi amehamishwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Maadili ya Jamii makao makuu ya jeshi hilo, Dodoma.

Nafasi ya Ng’anzi imerithiwa na aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, William Mkonda.

Sambamba na mabadiliko hayo, mkuu wa jeshi hilo, Camillus Wambura pia, amemhamisha aliyekuwa mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Dodoma, Boniphace Mbao kushika nafasi hiyo katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Katika Mkoa wa Kagera, watu saba walifariki dunia na wengine sita kujeruhiwa katika ajali ya lori lililogongana na Coaster na Toyota Hiace iliyotokea Desemba 3, mwaka huu.

Tukio lingine limetokea Desemba 6, mwaka huu, watu 16 wakiwamo wabunge na maofisa wa Bunge walijeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kwenda kwenye michezo Afrika Mashariki kupata ajali.

 Desemba 12 mwaka huu, watu wawili akiwamo kungwi walifariki dunia katika ajali ya lori lililogongana na bobaboda Handeni mkoani Tanga.

Desemba 18 mwaka huu, watu 15 walipoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari aina ya Coaster iliyogongana na lori la mizigo, Mikese mkoani Morogoro.

Hali kama hiyo, ilishuhudiwa mwisho wa mwaka jana. Desemba 5, 2023 ilitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu wanne huku wengine 21 wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu Bukoba mkoani Kagera.

Katika mwaka huo huo, Desemba 28 2023, watu watatu walihofiwa kufariki kwenye ajali ya gari iliyotokea eneo la Mbwewe wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Watu wanane waliokuwa wakisafiri na gari ndogo aina ya Probox Succeed maarufu kama mchomoko, walifariki dunia papo hapo na wengine sita kujeruhiwa baada ya gari hilo kugongana uso kwa uso na gari ya Kampuni ya Chicco.

Ajali, mabadiliko kikosi cha usalama barabarani

Baadhi ya wadau waliozungumza na Mwananchi leo Jumapili, Desemba 22, 2024, wamedai kuwa, uamuzi wa kufumua kikosi cha usalama barabarani umelenga kuonyesha uwajibikaji wa Jeshi la Polisi katika kipindi chenye mfululizo wa matukio ya ajali, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda.

Amesema katika nyakati hizi ambazo matukio ya ajali yanafululiza, kwa namna yoyote lazima kionekane kitu kinafanyika kwa kuwa, ni falsafa ya uwajibikaji.

“Kwa sababu ajali zinatokea, ili kuonyesha uwajibikaji, lazima Jeshi la Polisi lifanye mabadiliko maana kama ajali zinatokea haiwezekani yule kamanda aendelee kubaki pale pale, ingawaje hilo linaweza lisifungamane na sababu za kuondolewa kwake,” amesema Dk Mbunda.

Mbali na uwajibikaji, mwanazuoni huyo amehusisha wimbi la matukio ya ajali za barabarani na utegemezi wa barabara zaidi kama njia ya usafiri.

“Naamini kutegemea sana barabara kuna madhara makubwa na kunasababisha ajali ambazo tungeziepuka kama tungewekeza katika matumizi ya miundombinu mingine mfano reli tuliyonayo ingekuwa inakwenda hadi mikoa mingine, tungepunguza watu kulazimika kuendesha hadi nyumbani, wangetumia treni,” amesema Dk Mbunda.

Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamata), Majura Kafumu amehusisha wimbi la matukio hayo kila Desemba na ongezeko la vyombo vya usafiri vinavyotumia miundombinu ile ile.

“Desemba mahitaji ya matumizi ya barabara ni makubwa kuliko ukubwa wa barabara zenyewe. Watumiaji ni wengi kwa sababu mwaka mzima mtu hakwenda nyumbani ameahidi atakwenda mwisho wa mwaka.

“Kwa kuwa amenunua gari atakwenda nalo akaonyeshe nyumbani na hataenda peke yake anabeba na familia yake, kumbuka huyu mtu hana uzoefu wa kuendesha masafa marefu,” amesema Kafumu.

Katika kipindi cha Desemba, Kafumu amesema malori, mabasi ya kibiashara na magari binafsi ni mengi barabarani, jambo linalochochea kukithiri kwa ajali.

“Kuna kuchoka mwili, umeendesha hadi Iringa, umekula Iringa unaanza tena safari mwili ukiwa umechoka, wengine wanataka kunywa na bia moja au mbili. Njia huzijui, hawana uzoefu na safari za mbali, ukiweka kilevi maamuzi ni tofauti na ambaye hajanywa,” amesema Kafumu.

Amesisitiza inapofika mwisho wa mwaka watu wote wanahitaji kutumia njia zilizopo ambazo ni nyembamba, zisizo na viwango vya kimataifa.

“Jiulize mbona ajali nyingi hazitokei katika miezi mingine kwa sababu watu huwa makazini wakiendelea na shughuli zao,” amesema Kafumu.

Ili kudhibiti hali hiyo, Kafumu amependekea elimu itolewe kwa watumiaji wa gari binafsi kwenda taratibu na ikibidi wakodishe madereva kwa ajili ya kusafiri nao.

“Ukikodi dereva utakuwa na mamlaka ya kumzuia asinywe kilevi,” amesema Kafumu.

Related Posts