Ujerumani yachunguza maonyo kuhusu muuaji wa soko la Krismas – DW – 22.12.2024

Watu watano waliuawa, akiwemo mtoto mmoja, na takriban watu 200 walijeruhiwa, wakati mtu mmoja alipoendesha gari kwa kasi kupitia soko lenye msongamano wa watu la Krismasi katika mji wa Magdeburg, Ijumaa jioni.

Mshukiwa, daktari mwenye umri wa miaka 50 mwenye asili ya Saudi Arabia, ambaye ameishi Ujerumani kwa karibu miongo miwili na alikuwa na kibali cha ukaazi wa kudumu, yupo kizuizini kabla ya kuanza kwa kesi kwa tuhuma za mauaji, jaribio la mauaji, na kusababisha majeraha makubwa ya mwili.

Alitumia njia za dharura zisizo na vizuizi kuendesha gari kwa kasi kupitia soko la Krismasi, akiwagonga watu kwa mwendo wa kasi. Wanawake wanne wenye umri wa miaka 45, 52, 67, na 75, pamoja na mvulana mwenye umri wa miaka 9, waliuawa, mamlaka zilisema.

Wachunguzi wanasema mshukiwa alitenda peke yake lakini bado wanajaribu kubaini nia yake.

Berlin | Mkuu wa BKA, Holger Münch
Mkuu wa polisi ya uchunguzi wa uhalifu ya Ujerumani Holger Münch amesema wanachunguza nini kilikwenda kombo kuhusiana na mshukiwa wa Magdeburg.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mamlaka Zilijua Nini Kumhusu?

Siku mbili baada ya shambulio hilo la gari, Ujerumani bado ilikuwa kwenye mshtuko na maombolezo. Hata hivyo, vyombo vya sheria vilikuwa vinakabiliwa na maswali kuhusu kile walichojua kuhusu dereva huyo na iwapo janga hilo lingeweza kuzuiwa. 

Mkuu wa Ofisi ya Shirikisho la Polisi wa Jinai (BKA), Holger Münch, alisema shirika lake lilipokea taarifa kutoka Saudi Arabia mnamo Novemba 2023, iliyosababisha maafisa kuanzisha uchunguzi dhidi ya mshambuliaji — aliyejulikana tu kama Taleb A, kulingana na sheria za faragha za Ujerumani. 

Soma pia: Tukio la Magdeburg: Idadi ya vifo yaongezeka, Kansela Scholz autembelea mji huo

Katika mahojiano na kituo cha utangazaji wa umma ZDF, alisema hatua “muhimu za uchunguzi” zilichukuliwa, lakini maonyo hayo hayakuwa mahususi.

“Alikuwa pia na mawasiliano mbalimbali na mamlaka, alitoa matusi na hata vitisho. Lakini hakuwa anajulikana kwa vitendo vya vurugu,” alisema Münch kuhusu daktari huyo. 

Aliongeza kuwa BKA itafanya mapitio kuangalia iwapo makosa yoyote yalifanyika katika namna uchunguzi ulivyoshughulikiwa. 

Ofisi ya Shirikisho la Uhamiaji na Wakimbizi (BAMF) ilisema ilipokea taarifa kumhusu Taleb A mwishoni mwa msimu wa kiangazi mwaka 2023.

Magdeburg baada ya shambulio dhidi ya soko la Krismas| Kansela Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, katikati, alitembelea Soko la Krismasi, ambapo gari liliparamia watu Ijumaa jioni, mjini Magdeburg, Ujerumani, Jumamosi, Desemba 21, 2024.Picha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

BAMF ilisema kupitia mtandao wa X kwamba ilipokea taarifa kumhusu mtu huyo kupitia mitandao yake ya kijamii na kwamba ilichukuliwa kwa uzito.

Hata hivyo, shirika hilo lilisema kuwa halina mamlaka ya kufanya uchunguzi wa utekelezaji wa sheria, kwa hivyo lilimwelekeza mtoa taarifa kwa wakala husika. 

Picha za skrini zinazosambaa mtandaoni zinadaiwa kuonyesha ujumbe uliotumwa kwa BAMF kutoka kwa mtu aliyekuwa na maonyo kumhusu Taleb A. Uhalisia wa picha hizo za skrini haukuweza kuthibitishwa na shirika la habari la dpa. 

Toleo la Jumapili la gazeti la “Welt” liliripoti kuhusu mwanamke aliyepeleka maonyo kumhusu Taleb A kwenye akaunti ya BAMF kwenye X mwishoni mwa 2023. 

Soma pia: Ni mwaka mmoja baada ya shambulizi la mjini Berlin

Mwanamke huyo alikuwa awali amejaribu kutoa onyo kwa polisi ya Berlin kuhusu mtu huyo — hata hivyo, barua pepe yake haikufika kwa sababu aliipeleka kimakosa kwa polisi ya mji uitwao Berlin nchini Marekani, gazeti hilo liliripoti. 

Hata hivyo, Taleb A alikuwa kwenye rada ya idara ya mahakama ya Berlin. Kulingana na vyanzo vilivyozungumza na dpa, ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma wa jiji hilo ilikuwa imemfungulia mashtaka kwa matumizi mabaya ya simu za dharura. 

Tom-Oliver Langhans, mkurugenzi wa polisi wa Magdeburg, alisema Jumamosi kuwa polisi ya jiji hilo pia ilikuwa imefungua malalamiko ya jinai dhidi ya Taleb A hapo awali. Kesi hiyo ilifunguliwa takriban mwaka mmoja uliopita na sasa ni sehemu ya uchunguzi wa shambulio hilo. 

Magdeburg baada ya shambulio katika soko la Krismas
Watu wakiwa wamewasha mishumaa katika Soko la Krismasi la Magdeburg, Ujerumani, Jumamosi jioni, Desemba 21, 2024.Picha: Michael Probst/AP/picture alliance

Magdeburg ni mji wenye wakazi wapatao 237,000 katika jimbo la Saxony-Anhalt, kilomita 130 magharibi mwa Berlin.

Mshukiwa ni mwanaharakati mkosoaji wa Uislamu

Taleb A alijulikana kama mwanaharakati aliyekuwa mkosoaji wa Uislamu. Ameshatoa madai yasiyo ya kawaida kwenye mitandao ya kijamii na mahojiano, akidai kwamba mamlaka za Ujerumani hazifanyi vya kutosha kupambana na Uislamu wa itikadi kali. 

Soma pia: Ujerumani kuimarisha ulinzi kwenye masoko ya Krismasi baada ya shambulio la Magdeburg

Hapo awali alikuwa mtetezi wa wanawake wa Saudia wanaotoroka nchi yao, lakini baadaye alitoa ushauri dhidi ya kutafuta hifadhi Ujerumani. Kwenye tovuti yake aliandika kwa Kiingereza na Kiarabu: “Ushauri wangu: usiombe hifadhi Ujerumani.” 

Siku 10 tu zilizopita, jukwaa la Marekani “RAIR”, linalojieleza kama shirika la msingi linalopinga Uislamu, lilichapisha mahojiano ya zaidi ya dakika 45 na daktari huyo.

Katika mahojiano hayo, alidai kwamba polisi ya Ujerumani inavuruga kwa makusudi maisha ya watafuta hifadhi wa Saudia waliokataa Uislamu.

Pia alijitambulisha kama shabiki wa mmiliki wa X, Elon Musk, na chama cha mrengo mkali wa kulia cha “Alternative for Germany (AfD)”, ambacho alisema kina malengo sawa na yake. 

Ujerumani Magdeburg 2024 | Soko la Krismasi baada ya shambulio la gari - waandamanaji wenye itikadi kali za mrengo wa kulia
Maafisa wa polisi wamesimama mstari wakati waandamanaji wa mrengo wa kulia wakiwa na bango na bendera wakati wa maandamano baada ya shambulio hilo.Picha: Christian Mang/REUTERS

Hata hivyo, kwa wakati huo huo, alijitambulisha kama mtu wa mrengo wa kushoto kisiasa.

Mapema sana kwa tathmini ya mwisho 

Münch aliiambia ZDF Jumamosi kuwa haiwezekani kusema kwa uhakika kwamba kitendo hicho kilikuwa na msukumo wa kisiasa, ingawa alikiri kuwa mshukiwa alionyesha mtazamo wa kupinga Uislamu na kushiriki katika shughuli kwenye majukwaa ya mrengo wa kulia. 

Soma pia: Scholz autembelea mji wa Magdeburg baada ya shambulio

Mwendesha Mashtaka Mkuu Horst Walter Nopens huko Magdeburg alihisi kuwa nia ya mshukiwa huenda ilikuwa kutoridhishwa na jinsi wakimbizi kutoka Saudi Arabia wanavyoshughulikiwa nchini Ujerumani.

Vyanzo vya usalama vya Saudi Arabia vimesema kuwa viliionya Ujerumani kuhusu mshukiwa huyo na vilikuwa vimeiomba Ujerumani kumrudisha nchini humo, lakini Ujerumani haikujibu ombi hilo. 

Wajerumani wakumbuka mwaka mmoja wa mashambulizi ya Berlin

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Walisema kuwa mtu huyo ni Mwislamu wa madhehebu ya Shia kutoka mji wa Al-Hofuf, mashariki mwa Saudi Arabia. Waislamu wa Shia ni wachache nchini humo, wakiwa takriban asilimia 10 tu ya wakaazi wa taifa lenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Sunni.

Taleb A alifika Ujerumani mwaka 2006. Shirika la habari la dpa limefahamu kuwa aliomba hifadhi mnamo Februari 2016 na alipata hadhi ya ukimbizi wa kisiasa mwezi Julai wa mwaka huo.

Related Posts