Umuhimu mapumziko ya mwisho wa mwaka kwa familia

Dar es Salaam. Desemba inatajwa kuwa kipindi cha watu kupumzika kwa watu kuchukua likizo na kwenda sehemu mbalimbali za mapumziko au kutembelea ndugu.

Wengi wanatumia kipindi hiki pia kujipanga kwa ajili ya kuanza mwaka mwingine vizuri kwa kuangalia vitu walivyokuwa wamevipanga mwaka unaomalizia ni kwa kiasi gani vimefanikiwa, sehemu gani iliyokwama na kitu gani wanaweza kufanya ili kufikia ufanisi huo.

Kipindi hiki pia mbali na kuwa na sikukuu, ofisi nyingi zinafungwa kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wafanyakazi wake kupumzika, kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka na familia zao.

Hali hii inatajwa na wanasaikolojia kuwa na msaada mkubwa katika kujenga utimamu wa akili, kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya afya ya akili kutokana na uchovu unaopitiliza.

Akizungumzia umuhimu wa mapumziko hayo , mwanasaikolojia, Seby Wisdom anasema mapumziko ya mwishoni mwa mwaka humsaidia mtu kupumzika na kufikiria upya malengo yake ya mwaka ujao, ili kuboresha utendaji wake.

Hii pia humwezesha kukutana na watu wanaoweza kumpa mawazo mapya kuhusu kazi yake na kumsaidia kushinda changamoto zinazomkabili kazini.

Kwa kufanya hivyo, mtu hupata mawazo mapya ya kujenga ambayo yanampa hamasa ya kuanza mwaka mpya akiwa na nguvu na ari ya kurudi kazini.

Kwa upande mwingine, anasema mtu ambaye haendi likizo, atakuwa na uchovu, ukosefu wa mawazo mapya na hata utendaji wake unaweza kudidimia, tofauti na yule ambaye alichukua muda wa kupumzika.

Seby anasisitiza kuwa mapumziko ya mwisho ya mwaka si lazima mtu aitumie kutembelea maeneo ya starehe, bali inaweza kuwa ni wakati wa kupumzika kutokwenda kazini na kutafuta uzoefu mpya sehemu nyingine.

Mwanasaikolojia Charles Nduku pia anasema likizo inampa mtu nafasi ya kupumzisha akili yake kutoka katika mazingira ya kazi ya kila siku, jambo linalomwezesha kuwa na nguvu mpya na mawazo mapya atakaporudi kazini.

Anaongeza kuwa kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika kunachosha akili, hali inayoweza kuwa hatarishi kwa afya ya akili. Kwa hiyo, likizo inampa mtu fursa ya kufikiria vitu vipya, kutuliza akili na kupata nguvu mpya.

Nduku anatoa mfano wa timu za mpira, ambazo zinaposafiri kwenda kucheza mechi za kimataifa, hutumia siku moja kufanya utalii na kutembelea mji wa mwenyeji ili kupumzika na kutuliza akili zao.

Hata hivyo, anasema kuwa hali hiyo si ya kawaida kwa wafanyakazi wote, kwa sababu baadhi hupenda kwenda likizo wakati wengine hawapendi.

Wasiopenda kwenda likizo wanadai kutokuwa na shughuli ya kufanya katika siku watakazopewa, jambo ambalo wanaona ni bora kuendelea kusalia kazini kwa ajili ya majukumu yao ya kila siku.

“Ukienda likizo huna hela ni mtihani, uamke asubuhi hadi jioni kwa siku labda 21 mnatumia tu hela bila kuingiza ni ngumu, labda kama ofisi zingekuwa zinatoa hela kwa ajili ya likizo hii ingetuhamasisha,” anasema Didas Mmanga, ambaye ni mfanyakazi katika moja ya kampuni.

Anasema kukosekana kwa hela ndiyo sababu ya wengi kusalia kazini vipindi vyote vya mwaka, huku akiongeza kuwa wakati mwingine kazini ndiyo sehemu yenye amani.

 Tofauti na yeye, Faida Mohammed anasema katika baadhi ya ofisi imekuwa ni ngumu kutoa likizo kwa wafanyakazi wake, jambo ambalo linawalazimu wao kubaki kazini kwa miezi 12 ya mwaka.

“Tunataka kwenda kupumzika, lakini nani anakuruhusu, ukiomba mapumziko ni kama umeongea neno baya, baadhi ya watu hawathamini kupumzika kwa wengine, wanachoangalia ni kazi zao kwenda basi,” anasema.

 Tofauti na wawili hawa, katika baadhi ya ofisi, wafanyakazi wamekuwa wakilazimishwa kutumia siku zao za likizo ipasavyo kutokana na kutambua thamani ya likizo.

 Mmoja wa wafanyakazi katika kampuni za kigeni analiambia Mwananchi kuwa ofisi yake imekuwa ikihakikisha kila mtu anapumzika kama inavyotakiwa katika vipindi vyote vya mwaka.

“Kama muda wa kazini umekwisha lazima muondoke, siku ambazo hupaswi kuja kazini hutakiwi kuwapo na muda wa mapumziko lazima uende kwa sababu wanaamini mtu hawezi kufanya kazi muda wote bila kuchoka,” anasema mtumishi huyo.

Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude, likizo ni kipindi cha kupumzika baada ya kujishughulisha na kazi kwa kipindi fulani na katika sekta rasmi likizo ni jambo la kisheria.

Ni sharti mfanyakazi apate muda wa kupumzika na kuendelea kulipwa, ndiyo maana kwa Kiingereza likizo huitwa Paid-Time-off/out (PTO).

“Ni sawa kuchaji betri ya simu ili iendelee kufanya kazi. Kwa mfanyakazi ni kipindi cha kuupa mwili nafasi ya kujijenga kisaikolojia, kiakili, kimwili na hatimaye atakaporejea kazini aweze kuzingatia kazi zake akiwa na afya timamu ya mwili na akili,” anasema Mkude.

Anasema katika mtazamo huo, likizo ina mchango kwenye kukuza uzalishaji wa mfanyakazi husika na hivyo kwenye sehemu husika ya kazi.

“Mara nyingine watu hutumia likizo kufanya shughuli zao binafsi za kuwajenga kiuchumi, kama kusimamia mashamba, ujenzi na biashara. Hizi kwa ujumla wake zinawajenga watu hao kiuchumi na jamii nzima,” anasema Mkude.

 Katika mtazamo huo, anasema likizo si kupoteza rasilimali muda, bali ni kufanya rasilimali watu iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi binafsi na wa jamii.

Likizo na sehemu za utalii

Wakati mitazamo tofauti juu ya likizo ikitolewa, kipindi hiki pia ni mahususi kwa watu kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii, ikiwemo mbuga za wanyama, fukwe na sehemu za makumbusho.

Kipindi hiki pia ndiyo kampuni mbalimbali zimeandaa safari kwenda kutembelea vivutio, ikiwemo kuweka vifurushi vya watu kukaa mbuga za wanyama kwa siku kadhaa ili kuwabadilishia mazingira watu mbalimbali.

Hapa ndipo safari za vikundi hufanyika zinazojumuisha familia kwenda ndani na nje ya nchi kwa wenye uwezo zaidi.

Lakini pia kipindi hiki huweza kutumiwa ipasavyo na wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata nafasi ya kujifunza vitu vipya, ikiwemo kupika, kufua, kupata nafasi ya kucheza michezo mbalimbali na kujumuika na familia.

Katika kipindi hiki cha likizo, kulingana na bajeti ya mzazi, anaweza kwenda katika mbuga za wanyama za karibu kama Mikumi kwa wakazi wa Morogoro, Saadani kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na Pwani, Ngorongoro na Serengeti kwa watu kutoka eneo lolote.

Hata hivyo, kusimama peke yako kufanikisha safari hii inaweza kuwa changamoto, lakini mkiwa kama kundi inaweza kusaidia kupunguza gharama za wewe na familia yako kufanikisha azma hii.

Safari hizi za vikundi mara nyingi huandaliwa na kampuni mbalimbali, huku zikitoa ofa kwa familia inayotaka kujiunga nao katika safari hiyo.

Related Posts