Umuhimu wa kukumbuka uchumba katika ndoa

Kwa wale waliooa au kuolewa kabla ya ujio wa mitandao ya kijamii, watakumbuka picha ziwe za kupiga au zilizonasa kwenye bongo zao za uchumba wao. Japo ni matukio yaliyopita, yana umuhimu katika kudumisha au kunusuru ndoa.

Bila kumbukumbu, hakuna leo na leo ni kumbukumbu ya yaliyopita. Kwa nini tunasema kukumbuka uchumba ni muhimu katika ustawi wa ndoa? Kwanza, huleta furaha na hazina fichi katika mioyo yetu, hasa pale tunapokwazika au kuanza kuchokana. Wakati mwingine kumbukumbu huja kwa sababu ya furaha tu au mazoea.

Mnaweza kuwaona wanandoa au kupita sehemu fulani na kukumbuka uchumba wenu. Mnaweza kusikia wimbo hata kuona tukio fulani mkakumbuka uchumba wenu na kuondoka kwenye mtanziko au karaha mliyokuwa nayo kuhusiana na mahusiano na ndoa yenu.

Pili, huamsha upendo upya, hasa ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha uchumba ndipo mapenzi ya kweli yanapochipua, kuota hata kushamiri.

Fikiria ilikuwaje wakati mnakutana mlipoanza uchumba. Mlipenda kukutana wapi, kula chakula au kunywa kinywaji gani? Mliangaliana vipi? Mlikuwa mkikutana mara ngapi? Mliandikiana barua, whatsapps na kutumiana picha ngapi na za aina gani?

Tatu, kumbukumbu ya uchumba siyo tu hukumbusha, kuamsha furaha, hisa, na ridhiko mlivyopata, pia hutoa fursa ya kujitathmini na kujua wapi kuna upungufu au kwenye kuhitaji marekebisho au kuzingatia. Nne, kumbukumbu ya uchumba huhuisha ndoa. Wengi mtashangaa kuwaona wanandoa wazee hasa babu na bibi zetu wakisifiana kiasi cha kushangaa. Hii ni kwa sababu ya kumbukumbu walizotunza kwenye bongo zao.

Mnaweza kuwaona kama watu waliozeeka, kuchujuka hadi nyuso kujikunja. Ila muelewe. Wanachoona baina yao siyo mnachoona. Wao wanaonana kwa kutumia kumbukumbu za walivyokuwa wakati wa ujana wao.

Chukulia mfano mwanandoa ambaye ana kipara au mapengo. Hivi vitu haviepukiki na hutokea kadiri tunavyokua. Japo vitu hivi haviepukiki, kumbukumbu za uchumba huviweka kando na kuchukua nafasi ya kila kitu.

Je, unakumbuka muziki uliopigwa wakati wa harusi yenu kwa wale waliobahatika kufanya harusi? Je, unakumbuka chakula mlichopenda wakati wa uchumba? Vipi kuhusu sehemu mliyopenda kutembelea? Kwenye muziki, hili huitwa old is gold. Nini maana yake? Maana yake ni kumbukumbu za mambo tuliyofanya kwa ufanisi na furaha kama uchumba.

Maana, bila uchumba hakuna ndoa.

Nne, maisha ni kumbukumbu. Wangapi wanakumbuka nyakati wakiwa wanasoma? Wangapi hukumbuka mahafali yao, yawe ya shule ya msingi, sekondari, vyuo hata kuanza kazi? Nani asiyewakumbuka watu waliomzaa, aliozaliwa nao, waliosoma na kukua naye? Hivi vitu haviepukiki na ndivyo hufanya maisha yawe na maana na mvuto kama yalivyo. Na ndoa kadhalika, hasa vipindi vya uchumba, harusi, honeymoons kwa wale waliobahatika kwenda, mengine mengi bila kujali mahali, nafasi, umri hata nyadhifa.

Tunaoishi ughaibuni, huwa tunakumbuka karibu kila kitu cha nyumbani kuanzia hali za hewa, vyakula, mavazi, watu, siasa, miziki, harufu, mabonde, milima, mito hata wadudu.

Ndiyo maana kila mtu hupenda kwao na hakuna asiye na kwao. Kadhalika, na ndoa ina kwao na mambo yake ya kukumbuka. Hata walioishi au kukulia sehemu nyingi wanayo sawa na waliofunga au kuvunja ndoa nyingi. Hivyo, tumalizie kusisitiza kuwa kumbukumbu za uchumba ni mojawapo ya mambo yanayoweza kuwasaidia katika kutatua migogoro katika ndoa, hata kujifurahisha na kujiburudisha mbali na kujikumbusha na kujihuisha au kuwa wapya kwa kitambo fulani.

Kwa Watoto wa kwanza, kama tunavyokumbuka wazazi wetu walipokuwa vijana wakati tukizaliwa, ndivyo hivyo wanandoa wanavyokumbuka uchumba wao. Je ni kwanini? Japo kuna majibu mengi, mojawapo ni kwamba kipindi cha uchumba ndicho kipindi cha kuweka msingi wa ndoa madhubuti na fanisi.

Tuweke wazi. Kwa wale walioibana au kukutana sehemu zisizofaa au kufurahisha kama udangaji, kunaweza kukosekana kumbukumbu ya maana. Hata hivyo, kama mtajikuta katika kundi hili hasa wale walioona kwa mtindo wa njoo tukae baadaye ikawa ndoa­­­­ bado wanacho au wanavyo vitu vya kukumbuka.

Kama siyo mandhari, basi kumbuka hata mavazi mliyovaa, picha mlizopiga au kutunza kwenye nyoyo zao. Kila mtu ana kumbukumbu ziwe mbaya au nzuri. Hapa, tunasisitiza kumbukumbu tunazomaanisha na kushauri ni zile zenye kuwapendeza.

Related Posts