Urusi imeshuhudia wimbi la majaribio ya matukio ya kuwashwa moto yakilenga mabenki,vituo vya biashara, ofisi za posta na majengo ya serikali.
Matukio hayo yameonekana kufanyika katika kipindi cha siku tatu zilizopita ikielezwa kwamba takriban matukio 20 tofauti yamerikodiwa, ya watu kujaribu kuwasha vifaa vya miripuko au kuwasha baruti katika majengo tangu Ijumaa hasahasa kwenye miji ya Saint Petersburg,Moscow na vitongoji vya maeneo hayo kwa mujibu wa shirika la habari la serikali TASS na mtandao huru wa habari Fontanka.
TASS limenukuu chanzo cha usalama ambacho hakikutajwa,likisema wanaofanya matukio hayo ni watu waliolipwa na kundi la wahalifu kuendesha mashambulio hayo.
Picha za video zilizonaswa na kamera za uchunguzi katika baadhi ya maeneo zilizosabambazwa kwenye mitandao ya kijamii,zinaonesha watu kadhaa wakitumia simu za mkononi kurekodi matukio ya kuanzisha moto.
Katika moja ya matukio hayo picha zinaonesha athari za shambulio lililoharibu mashine ya kutowa pesa ATM na kuripuka kwa madirisha kadhaa kwenye jengo la karibu,huku picha nyingine zikionesha gari la polisi limeteketezwa.
Ripoti zinasema mashambulio yamekuwa yakilenga mashine za kutowa pesa za mabenki yanayoendeshwa na serikali, vituo vya biashara,ofisi za posta,ofisi za shughuli za kijeshi,magari ya polisi na majengo mengine ya shughuli za kiserikali.
Benki ya mikopo inayosimamiwa na serikali ya Sberbank imeripoti kuongezeka kwa asilimia 30 matukio ya majaribio ya kuchoma moto taasisi hiyo katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Taarifa hiyo imeripotiwa na shirika la habari la RIA Novosti ambalo limenukuu kitengo cha habari cha benki hiyo.
Shirika la habari la TASS limeripoti kwamba wengi wa waliokamawa kufuatia matukio hayo ni wastaafu huku benki ya Sberbank ikisema watu hao wamesajiliwa na wahalifu walioko nchini Ukraine.Soma pia: Urusi yapuuza sheria ya kudhibiti silaha
Kitengo cha usalama cha Moscow awali kiliwatahadharisha wananchi wa Urusi kwamba wahalifu wanaofanya udanganyifu kutoka Ukraine,wanaojifanya kuwa mawakala wa usalama wamekuwa wakiwapigia simu wastaafu/wazee raia wa Urusi na kuwataka washiriki kufanya matukio ya kuteketeza maeneo kwa ahadi ya kuwalipa pesa au kuwafungulia tena akaunti zao zilizofungwa.
Serikali mjini Kiev bado haijatowa tamko kuhusu wimbi hilo la visa vya uteketezaji maeneo nchini Urusi au tuhuma zilizotolewa, zikidai matukio hayo yanachochewa kutoka ndani ya Ukraine.
Ofisi chungunzima za kijeshi za Urusi zimeshambuliwa kwa mabomu ya kutengenezwa kienyeji ya Molotov tangu nchi hiyo ilipopelewa wanajeshi wake Ukraine Februari 2022.
Majengo mengi ya ofisi za usajili wa wanajeshi,yalijikuta kulengwa kwa kiasi kikubwa katika matukio hayo baada ya rais Vladmir Putin mwaka 2022 kutangaza sheria ambayo haina uungwaji mkono mkubwa nchini humo iliyoshuhudia zaidi ya warusi 300,000 wakilazimishwa kwenda kupigana vitani,Ukraine.
Mahakama za Urusi zimetowa hukumu za vifungo vya miaka mingi jela kwa wale waliokamatwa kwa kuhusika na mashambulio hayo.