Uwekezaji mkubwa waanza jengo kubwa la kibiashara Dodoma

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), unatarajia kufanya uwekezaji mkubwa katika Jiji la Dodoma kwa kujenga jengo la minara miwili ambalo litachochea ukuaji wa uchumi na utalii katika jiji hilo. Jambo limepongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule. Akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti katika kiwanja namba 3 kitalu F, kilichopo Njedengwa jijini Dodoma.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema ujenzi wa mradi huo mkubwa utachochea ukuaji wa uchumi na utaleta heshima katika Kanda ya Kati na Taifa kwa ujumla. Pia amesema moja wapo ya vitu ambavyo Rais anatamani kuviona ni kuona Mkoa wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya Nchi unaleta mikutano ya kimataifa, hivyo ujenzi wa jengo hilo la kitega uchumi la NSSF linaendana na azma ya Serikali ya awamu ya sita ambayo inaendelea kuufungua mkoa huo pamoja na maeneo mengine nchini.

Awali akizungumza katika eneo hilo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. Mshomba amesema NSSF imeamua kuwekeza katika mradi huo kwa sababu shughuli za uwekezaji ni jambo la msingi na wamekuwa wakiwekeza kwenye maeneo tofauti tofauti ili kuhakikisha thamani ya michango ya wanachama haipotei na kupata faida inayoiwezesha Mfuko kulipa mafao kwa wanachama wake.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Mhandisi Helmes Pantaleo, Meneja Usimamizi wa Miradi NSSF, amesema mradi huo unatarajiwa kujengwa jengo la ghorofa 16 na kuwa umegawanyika sehemu tatu ikiwemo ya ofisi, hoteli na maduka makubwa.

Related Posts