Wasiojulikana wavunja vibanda 12 vya biashara, wapora mali

 Musoma. Watu wasiojulikana wamevamia na kuvunja zaidi ya vibanda 12 vya maduka katika eneo la Kariakoo, Manispaa ya Musoma, mkoani Mara na kupora mali mbalimbali.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, Desemba 22, 2024. Watu hao ambao idadi yao bado haijafahamika, wanadaiwa kuvamia eneo hilo na kubomoa makufuli ya vibanda hivyo na kuiba mali zilizokuwamo.

Tukio hili limetokea siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi kuagiza Jeshi la Polisi kufanya doria za usiku na mchana katika maeneo yote wanayoishi wananchi kwa lengo la kuwalinda raia na mali zao, hasa katika msimu huu wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Mmoja wa wamiliki wa vibabda hivyo, Marko Machere ameiambia Mwananchi Digital leo Jumapili Desemba 22, 2024 kuwa alipokea simu asubuhi kutoka kwa watu waliomweleza kuwa vibanda vyao yamevunjwa.

“Baada ya kufika ni kweli tumekuta vikiwa wazi na kufuli zikiwa zimevunjwa na mali zilizokuwepo dukani zimeibiwa, kwa kweli hii ni hasara kubwa sana kwetu, mimi nauza nguo na kama unavyojua huu ndio wakati wa kupata wateja wengi wanaonunua nguo hasa za watoto kwa ajili ya sikukuu,” amesema Machere,

Amesema katika tukio hilo ameibiwa mzigo wenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni aliouingiza jana jioni.

Hata hivyo, amesema bado hajajua thamani halisi ya vitu vilivyoibiwa huku akiliomba jeshi la polisi kufanya doria katika maduka yaliyopo pembezoni na mitaani badala ya kufanya doria katika barabara kuu peke yake.

“Kumeibuka makundi ya vijana ambayo tunadhani ndio wamehusika na tukio hili, wana tabia ya kutembea na mapanga na wanapora watu simu, tayari tumetoa taarifa polisi juu ya uwepo wa makundi haya mtaani, tunashukuru tayari polisi wamefika hapa asubuhi na wameahidi kurejea tena jioni kwani tukakuwa na kikao kwaaj ili ya kujadili suala la ulinzi  na usalama,” amesema Machera.

Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo ambaye amesema bado hajapata taarifa kuhusu tukio hilo na ameahidi kufuatilia na atalitolea taarifa baadaye.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema tayari vyombo vya dola vimeanza kushughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuanza uchunguzi.

Amesema hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

“Polisi wamefika pale wamechukua taarifa kwa ajili  ya kuanza uchunguzi lakini watakwenda kukutana na wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo kujadiliana kuhusu masuala ya ulinzi na usalama, kwenye kikao hicho pia watakuwepo viongozi wa serikali za mitaa  wa eneo husika na diwani wao,” amesema Chikoka.

Amesema pamoja na mambo mengine, wamebaini kuwa licha ya eneo hilo kuwa na maduka mengi, lakini halina ulinzi wa kutosha.

Chikoka amesema taarifa alizozipata, eneo hilo lina mlinzi mmoja pekee hali iliyowafanya wezi hao kutekeleza tukio hilo la kihalifu kirahisi.

Related Posts