Wenye ulemavu wa kupitiliza kufundishwa wakiwa nyumbani

Rombo. Serikali imeanza utekelezaji wa usajili wa mwongozo wa watoto wenye ulemavu unaowapa nafasi wale wenye changamoto zaidi kufundishwa wakiwa nyumbani.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Desemba 22, 2024 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akikabidhi viti mwendo kwa watoto wenye mahitaji maalumu wilayani humo.

Amesema Serikali haitamwacha mzazi abebe jukumu la mtoto mwenye ulemavu peke yake, hivyo hakuna haja ya kuwaficha wenye changamoto hiyo nyumbani.

Profesa Mkenda amewataka maofisa ustawi wa jamii waliopo maeneo yenye watoto hao kutoa taarifa ili kuwabaini wenye changamoto zaidi ili wasaidiwe.

“Wale watoto wenye changamoto kubwa zaidi na wazazi hawataki watoke nyumbani tuna mwongozo wa kusoma akiwa nyumbani kwake, tutakuja kumfundisha mtoto nyumbani na tayari tumesajili kutekeleza maelezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye katika sekta ya elimu ataacha alama itakayodumu,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anasoma kwa kuwa imefanya uwekezaji katika sekta ya elimu.

Pamoja na mambo mengine, Profesa Mkenda amesema ni marufuku mwanafunzi yeyote kurudishwa nyumbani kwa sababu mzazi hajatoa mchango wa shule.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amesema kwa sasa wameanza kuchapisha vitabu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu hasa wale wasioweza kusoma kwa macho, watasoma kwa kutumia vidole.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu vitabu vyote tunavyochapisha sasa hivi tunachapisha  nakala zenye maandishi yaliyokuzwa na vingine vyenye maandishi ya nukta nundu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala amesema kwa kuwa eneo hilo lina watoto wengi wenye mahitaji maalumu, hivyo wazazi hawapaswi kuwaficha.

“Sitarajii kuona mtu anamficha mtoto ndani, hawa ni ndugu zetu, wana haki zote sawa na wengine, hawatakiwi kutofautishwa na mtoto yeyote,” amesema.

Related Posts