Baraza la katiba nchini Msumbiji, muda mfupi uliopita limeyaidhinisha matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi, mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo.
Umma wa Msumbiji uko katika hali ya wasiwasi baada ya muda mfupi uliopita baraza la katiba kutangaza kuyaidhinisha matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi Daniel Chapo, mgombea wa chama tawala cha Frelimo.
Mwandishi habari mjini Maputo,Markus Muledzera aliiambia Dw Kiswahili kwamba mjini Maputo ”Vifaa vya kivita vimewekwa tayari na hakuna mtu anayeweza kuingia au kutoka Maputo”
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane ameshawaambia wafuasi wake wajiandae kufanya maandamano makubwa yatakayolemaza shughuli zote nchi nzima kufuatia uamuzi huo wa baraza la katiba.
Mchambuzi ya masuala ya kisiasa na kiusalama aliyeko mjini Maputo Johann Smith kabla ya kutangazwa uamuzi wa baraza la katiba aliliambia shirika la habari la AFP kwamba miji mikubwa ikiwemo mji mkuu Maputo huenda ikawa chini ya mzingiro wa waandamanaji.
Awali mchambuzi huyo alisema anaamini kwa asilimia 100 kwamba baraza la katiba, litayaunga mkono matokeo yaliyompa ushindi Daniel chapo wa chama tawala cha Frelimo na kwamba damu lazima itamwagika nchini humo.
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume yalimpa ushindi Chapowa asilimia 71 huko Mondlane akipewa nafasi ya pili akitajwa kupata asilimia 20 ya kura, lakini mgombea huyo wa upinzani anadai yeye ndiye mshindi kwa mujibu wa zoezi jingine lililofanywa pembeni la kuhesabu kura linaonesha alipata asilimia 53 ya kura na chapo alinyakuwa asilia 36.
Mondlane amedai matokeo yalichakachuliwa kumpendelea mgombea wa Frelimo.
Ripoti zinasema kwamba maduka na maeneo ya biashara yamefunga milango yao na mitaa ya mji mkuu Maputo imebaki mitupu licha ya kwamba ni kilele cha kuingia kwenye msimu wa sikuukuu ya Krismasi.
Waandishi habari wa AFP wamesema barabara kuu za kuelekea katikati ya mji huo zimefungwa kwa vizuizi vya polisi huku zile za kuelekea ikulu na maeneo ya ofisi za baraza la katiba nazo zikiwa pia zimefungwa.
Nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika iko kwenye hali ngumu ya machafuko ya kisiasa tangu tume ilipotangaza matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 9 yaliyompa ushindi mgombea wa chama cha Frelimo ambacho kiko madarakani tangu mwaka 1975 nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wareno.
Soma zaidi: Msumbiji yasubiri uamuzi wa baraza la katiba kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais
Polisi wamekuwa wakituhumiwa kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji huku watu wapatao 130 wakiaminika wameuwawa kwa mujibu wa shirika la kiraia la Plataforma Decide ambalo takwimu zake ndizo zinazotumiwa na shirika la kutetea haki za binadamu la kimataifa la Amnesty International.