Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila leo tarehe 20 Disemba, 2024 amezindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke ambayo imeundwa ili kusimamia na kushauri shughuli zote za uendeshaji wa Hospitali hiyo.
“Dhumuhi la kuundwa kwa bodi hizi ni kumsaidia Mhe, Rais kuhakikisha wananchi wake wanapatiwa huduma bora, ni imani yangu na agizo langu kwamba bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke itakuwa chachu ya maendeleo ya Hospitali na kuleta mabadiliko chanya katika mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi”, Alisema Mhe. Edward Mpogolo Mkuu wa wilaya ya Ilala.
Akizungumza awali wakati akitoa taarifa fupi ya Hospitali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro amesema Hospitali hiyo imejitahidi kwa kiasi kikubwa kutumia mapato yake ya ndani kufanya maendeleo mbalimbali ikiwemo kuongeza huduma ambazo hazikuwepo kama vile vipimo vya CT Scan, Huduma za usafishaji damu na huduma nyingine nyingi zilizoboreshwa.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Hospitali ya Temeke Dkt. Deus Buma ameshukuru kwa kuteuliwa kwake kuiongoza bodi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ambapo amesema bodi hiyo ya ushauri itashirikiana na menejimenti ya Hospitali katika kuhakikisha inatimiza wajibu wake na kuisaidia Hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.