Fadlu ashindwa kujizuia, afichua ishu ya Mpanzu

SIMBA imesharejea Dar es Salaam tayari kwa mechi ijayo dhidi ya JKT Tanzania, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu David akikunwa na kiwango cha Ladack Chasambi na kufunguka kwa moto alioanza nao Ellie Mpanzu aliyemtumia kwa dakika 57 walipoizamisha Kagera Sugar kwa mabao 5-2, akisema akiizoea ligi itakuwa balaa.

Katika mchezo huo, Mpanzu alicheza kwa mara ya kwanza katika mashindano akiwa na uzi wa Simba, huku  Chasambi aliasisti mara tatu, wakati Steven Mukwala akifunga mara mbili wakati akiinyoa Kagera na kuirejesha timu hiyo kileleni mwa msimamo mwa Ligi Kuu ikiiengua Azam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu mekiri kukunwa na soka lililopigwa na timu nzima, huku akifurahishwa na mwenendo wa Chasambi ameonyesha na kiu ya kuhitaji nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi chake cha kwanza.

“Chasambi (Ladack) ameonyesha kiwango kizuri, na ni furaha kubwa kwangu kuona hilo kwa sababu ni kati ya wachezaji ambao naona wanakitu, anachotakiwa ni kuendelea kujituma ili kuonyesha kiwango chake kwa ukubwa zaidi,” alisema.

Kocha huyo alielez, ingawa Chasambi alikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara mwanzoni mwa msimu, alijitahidi kuboresha uwezo wake na sasa ni mchezaji muhimu katika kikosi cha kwanza cha Simba.

Pamoja na kuzungumzia kiwango cha Chasambi, Fadlu pia aliongezea kuhusu mchango wa wachezaji wengine na umuhimu wa kuhakikisha kila mchezaji anapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake. Alisema kuwa, ushindi dhidi ya Kagera Sugar ulikuwa ni matokeo ya jitihada za wachezaji wote.

Kama ilivyo kawaida kwa Fadlu, alizungumza kuhusu umuhimu wa timu kama ‘unit’ inayoshirikiana, na siyo tu kuhusu mchezaji mmoja. Alisisitiza kuwa, licha ya kwamba Chasambi alikua kivutio kikubwa katika mchezo huo, kila mchezaji alichangia kwenye mafanikio ya timu.

Akimuongelea Mpanzu katika dakika 57 ambazo alimpa kuichezea Simba kwa mara ya kwanza, Fadlu alisema taratibu mchezaji huyo atakuwa katika daraja moja na wenzake anachohitaji ni michezo zaidi ya ushindani.

“Akiizoea ligi atakuwa bora zaidi, kwani ni muda mrefu hajacheza, hivyo akicheza mara kwa mara na kupata ushindani atakuwa moto na kuisaidia timu akishirikiana na wenzake, kwani ana uwezo mkubwa,” alisema Fadlu.

Juu ya kiwango alichokionyesha Kaitaba Chasambi kwa upande wake, alisema alijifisika faraja na furaha kubwa kwa kuisaidia timu yake kupata ushindi muhimu.

“Huu ni ushindi wa timu nzima, sio wangu peke yangu. Tumepambana kama timu na kila mchezaji alichangia kwa namna yake. Kocha alitufundisha kuwa kila mchezaji lazima atumie nafasi yake vizuri, na leo (juzi) nilifanya hivyo,” alisema Chasambi.

Chasambi alikiri kwamba mwanzoni mwa msimu alikuwa na changamoto ya kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, lakini alisisitiza kuwa alikuwa akijitahidi kila siku kujitengenezea nafasi na kuongeza ubora wake.

Mabao ya Simba katika mchezo huo, yalifungwa na Shomary Kapombe, Jean Charles Ahoua, Fabrice Ngoma na Steven Mukwala akifunga mara mbili, mabao ya Kagera Sugar yalifungwa na Cleophace Mkandala na Peter Datius.

Katika misimu mitatu iliyopita, Simba ilivuna pointi mbili tu Kaitaba, inakumbukumbu ya kufungwa bao 1-0  Januari 26, 2022 na Hamis Kiiza ‘Diego’, alitoa sare Desemba 21, 2022 na Mei 12, 2024  ya bao 1-1 kwenye kila mchezo.

Simba itakuwa na uhakika kusherekea sikuu ya mwaka mpya kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa itashinda michezo yake miwili ijayo ambayo ni dhidi ya JKT Tanzania nyumbani Desemba 24 na mmoja ugenini dhidi ya Singida Black Stars Desemba 28 kwenye uwanja wa Liti.

Related Posts