Dar es Salaam. Ingawa baadhi ya watu hufikiri barafu husaidia kubana uke au kuongeza hisia za mapenzi, wataalamu wa afya wamesema matumizi ya barafu ukeni husababisha maambukizi na harufu mbaya sehemu za siri.
Wataalamu hao wameonya hayo kutokana na mjadala ulioibuka baada ya baadhi ya wanawake kupitia mitandao ya kijamii kushauriana kuitumia kwa lengo kubana uke, muda mfupi baada ya kushiriki ngono.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Chaurembo aliandika ”Umetoka kuchepuka halafu ukarudi nyumbani mpenzi wako akahitaji tendo wakati huo, jinsi ya kufanya chukua barafu weka itabana kama haijawahi kuguswa,” aliandika.
Kauli hiyo ilipata uungwaji mkono wa wanawake mbalimbali, huku wengine wakiomba ufafanuzi zaidi muda gani waweke na kwa kiwango gani itahitajika.
Ruth Zablon, akizungumzia njia hiyo amesema ni miongoni mwa mbinu wanazotumia wanawake wengi kutengeneza maumbile yao.
“Zipo njia nyingi sio barafu tu, wengine wanatumia maji ya moto kujikanda au mvuke. Japo situmii, ila wanaotumia wanapata matokeo waliyotaraji kwa muda wanaotaka,” amesema.
Hata hivyo, wataalamu wa uzazi na afya ya jamii wameonya matumizi ya njia hiyo wakisema haisaidii kitu chochote badala yake ni kujitafutia matatizo sehemu za uzazi.
Mtaalamu mshauri wa masuala ya afya ya jamii, Festo Ngadaya amesema barufu inapowekwa kwenye ngozi ya uke sehemu hiyo hutengeneza joto kukabiliana na hali hiyo ya ubaridi.
“Ukiweka barafu ukeni ngozi itakaza, lakini inarejea kwenye hali yake baada ya muda mfupi mwili ukishajitengenezea joto kukabiliana na huo ubaridi, sehemu za siri za mwanamke huitaji joto, ukiweka barafu unakwenda kutengeneza madhara,” amesema.
Ngadaya amesema ndani ya uke wapo bakteria rafiki wanaolinda eneo hilo, barafu inapowekwa eneo hilo inakwenda kuvuruga makazi yao na kuwageuza bakteria hao kuushambulia mwili badala ya kuulinda.
Baada ya kutokea kwa hali hiyo, tindikali iliyopo ukeni hubadilika na kuanza kutoa harufu mbaya sehemu za siri na majimaji machafu.
Mbali na barafu, Ngadaya amesema wapo wanawake wengine huweka limao ndani ya uke ili kukaza misuli ya uke, akisisitiza ni tabia ya kuepukwa.
“Limao lina asidi, unapoiweka ukeni unakwenda kuwaathiri hao walinzi wa mwili ambao ni bakteria salama, wanapoondoka ukeni utasikia malalamiko ya baadhi ya watu kupata harufu mbaya ukeni,” amesema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi, Dk Andrew Foi akizungumzia tabia hiyo amesema ni hatari kuweka barafu sehemu za siri.
“Ngozi ya uke ni tofauti na maeneo mengine, kuweka barafu ni kubadili mazingira ya bakteria wanaoishi ukeni kitendo ambacho ni kutengeneza mazingira ya kuotesha wadudu wabaya mwilini,” amesema.
Naye Dk Naniel Nkungu, mbobezi wa afya ya uzazi amesema barafu hutumiwa kupunguza maumivu kwa watu walioumia na sio ukeni.
“Kama mtu ana shida ya kiafya wamuone daktari, si sahihi kuweka barafu sehemu za siri na haisaidii kitu, bali ni kutengeneza matatizo mengine,” amesema.
Mtalamu mwingine wa masuala ya uzazi, Dk Thomas Kakumbi amesema matumizi ya barafu maeneo ya uke mara nyingi hutumiwa na wanawake waliojifungua kupoza maumivu sehemu ya nyonga.
“Sasa wengine wanatumia kuongeza ladha ya tendo la ndoa, kurejesha bikra baada ya tendo husika sio barafu tu, sisi wataalamu tunashuhudia mambo mengi wapo wanaoweka pipi kifua, karafuu na si kwamba vitu hivi vinasaidia, hapana.
“Vitu vingine vinavyotumika ni kujifukuza udi, vitunguu saumu, kujifukiza mvuke,” amesema.
Dk Thomas amesema tabia hiyo ina madhara na wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza via vya uzazi vya mwanamke visiwekwe kitu chochote.
Amesema uke hujisafisha wenyewe na haupaswi kusafishwa kwa kitu chochote.
Mtaalamu huyo amesema ndani ya uke kuna ‘acid’ inapaswa kuwepo, ili uke uendelee kuwepo bila kuwa na madhara yeyote.
“Sasa chochote kitakachoingia na kubadilisha hali ya ‘acid’ ukeni, kunaleta madhara, ikiwemo uwepo wa fangasi ukeni na bakteria wa aina tofauti ambao watu huita U.T.I sugu,” amesema.
Amesema tatizo kubwa endapo vitu hivyo vinavyoshauriwa kutoingizwa ukeni vikiendelea kutumika, mhusika kupoteza uwezo wa kupata ujauzito na kupitia maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.
Fanya haya kuimarisha afya yako
Kupitia jarida la afya mtandaoni ‘Zulu Medics Cosmetics’, Dk Jeane Lombard wa nchini Afrika kusini amebainisha njia mbili za kuurejesha uke kwenye hali yake, ikiwemo kufanya upasuaji.
Upasuaji huo ni wa kukaza eneo la uke na njia nyingine ni kufanya mazoezi ya nyonga.
Ameshauri kuepukwa matumizi ya maji ya moto kukaza eneo la uke, mvuke, mafuta ya tufaa, alovera, dawa ya meno au vilevi vyovyote.