Jean Baleke ameyatimba Yanga | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Jean Baleke hana nafasi katika kikosi cha timu hiyo tangu enzi za kocha Miguel Gamondi na hata sasa timu ikiwa chini ya Sead Ramovic akishindwa kabisa kumtumia katika mechi za Ligi ya ndani na ile ya Mabingwa Afrika.

Lakini sasa unaambiwa jana ni kama ameyatimba na kujiweka katika nafasi finyu ya kuendelea kusalia katika kikosi hicho, kwani kwa sasa wanasubiri maamuzi ya mabosi wa klabu hiyo ili kumbakisha Jangwani.

Ipo hivi. Nyota huyo wa zamani wa Simba, aliyetokea TP Mazembe ya DR Congo amejiweka karibu na mlango mgumu wa kutokea baada ya kukacha mazoezi ya timu hiyo.

Baleke hajaonekana ndani ya kambi ya Yanga kwa zaidi ya wiki moja akikosa ratiba zote za mazoezi ya timu hiyo huku pia hata uwanjani akikosekana.

Mara ya mwisho kwa Baleke kuichezea Yanga ilikuwa Novemba 30, 2024 alipokuwa benchi kwenye kikosi kilichocheza mchezo wa ugenini dhidi ya Namungo na mabingwa hao wakishinda kwa mabao 2-0.

Mshambuliaji huyo alikuwa katika msafara wa Yanga ikiifuata MC Alger ya Algeria kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini hakukaa hata benchi.

Baada ya hapo Baleke ambaye anaichezea Yanga kwa mkopo hajaonekana tena kwenye kikosi cha Yanga.

Taarifa za ndani kutoka Yanga ni kwamba mshambuliaji huyo anapigiwa hesabu za kuachwa baada ya makocha wote kushindwa kuelewa kiwango chake.

Sio tu kwa kocha Sead Ramovic, lakini Baleke alishaanza kukutana na wakati mgumu hata kwenye utawala wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi.

Yanga inataka kuachana na Baleke kwenye dirisha hili dogo la usajili ili waingize mshambuliaji mwingine wa maana ambaye kocha Ramovic na mabosi wake wapo msituni kumsaka.

Yanga haitamsajili tena mshambuliaji Mganda Fahad Bayo ambaye licha ya kufanya majaribio kwa muda mrefu lakini kiwango chake kimeshindwa kuwashawishi makocha wa timu hiyo.

“Hatuwezi kuendelea na Baleke, tulikuwa na matarajio makubwa lakini mambo yamekuwa tofauti unajua shida malalamiko ya makocha wote ni kwba kiwango chake hakiwaridhishi kuanzia mazoezini,”alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga.

Juzi mshambuliaji huyo alionekana makao makuu ya klabu hiyo Jangwani ikielezwa alikuwa na kikao muhimu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine ilitajwa ilikuwa ni hatua ya kujua mustakabali wake.

Tangu atue Yanga, Baleke licha ya kukosa mechi nyingi amefanikiwa kufunga bao moja pekee alilowafunga Coastal Union, timu yake ikishinda kwa bao 1-0 pekee.

Related Posts