Jinsi kesi hizi zilivyotikisa | Mwananchi

Dar es Salaam. Mahakama ni mojawapo ya mihimili ya dola yenye dhamana ya kusimamia utoaji haki nchini.

Inatekeleza jukumu hili kwa kupokea, kusikiliza, na kuamua kesi mbalimbali za madai na jinai za aina zote zinazowasilishwa mbele yake.

Mwaka 2024, Mahakama ya Tanzania imepokea na kusikiliza kesi nyingi katika ngazi mbalimbali nchini kote.

Baadhi ya kesi hizo kubwa, zenye masilahi mapana kwa umma, zimeibua mijadala katika jamii.

Kesi hizi zimehusisha watu maarufu wakiwamo wanasiasa, maofisa na watumishi wa umma, wafanyabiashara na zingine zenye upekee wa mashtaka au madai na zile zinazogusa masilahi ya umma kwa jumla.

Baadhi ya kesi zilizofunguliwa na ambazo bado zinaendelea mahakamani katika hatua mbalimbali ni kesi ya meya mstaafu Boniface Jacob maarufu Boni Yai.

Hizi ni kesi za jinai dhidi ya mwanasiasa huyo maarufu nchini, aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa za Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam.

Jacob, anakabiliwa na kesi mbili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu za kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii, moja yeye na mwenzake, mwanaharakati Godlisten Malisa na nyingine  pekee.

Anadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika machapisho hayo anatuhumiwa kuwahusisha maofisa wa polisi na vifo vya raia.

Katika kesi ya kwanza, Boni Yai na Malisa walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 6, 2024 na kusomewa mashtaka matatu, mawili ya Boni Yai na moja la Malisa, wakidaiwa kutenda makosa hayo Machi 19, 2024, Aprili 13 na Aprili  22, 2024.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024, wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo kuwa Jeshi la Polisi linaua raia, wakilihusisha na kifo cha mwananchi mmoja, Robert Mushi, maarufu Baba G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo.

Katika kesi ya pili, Boni Yai pekee anakabiliwa na mashtaka mawili, akidaiwa kuwahusisha Wakuu wa Upelelezi wa Kanda ya Dar es Salaam na wa mikoa mingine, utekaji na mauaji ya raia.

Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai (kulia) na mwenzake Godlisten Malisa wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yao ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii, kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka hayo Septemba 19, 2024, akidaiwa kutenda makosa hayo  Septemba 12 na 14, 224 jijini Dar es Salaam.

Kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa

Hii ni kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili, Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, mkazi wa Mbezi; katika Mahakama ya Kisutu.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 25517/2024, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu wenye asili ya  China, namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.

Wanadaiwa kuwa Desemba 21, 2022, Mkama na Nyabuya walitengeneza nyaraka ya kughushi  yenye kichwa cha habari ‘’Nyongeza ya Msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.

Barua hiyo ya Desemba 21 mwaka 2022,  iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.

Ingawa walitekeleza sharti la kulipa Sh45 milioni, hawakuwahi kutolewa gerezani humo, hadi mmoja wao alipotembelewa na wakili wake akamuonesha barua hiyo na alipoifuatilia ndipo ikabainika kuwa ni ya kughushi.

Kesi ya Derick, kutishia kwa bastola Club 1245

Hii ni kesi ya jinai inayomkabili mkazi wa Salasala jijini Dar es Salaam, Derick Derick Junior (36), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni iliyoko Kinondoni.

Anakabiliwa na mashtaka mawili, kujeruhi na kutembea na silaha hadharani kwa namna ya kuleta utisho, akidaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 27, saa 12.30 asubuhi, katika Klabu ya Usiku (Night Club)1245, eneo la Masaki wilayani Kinondoni.

Anadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio alimjeruhi Julian Bujuru kwa kumpiga kwa kitako cha bastola na kumjeruhi usoni (sehemu ya hicho na puani) na kwamba alitoa silaha na kumtishia Bujuru, kitendo ambacho kinatishia amani kinyume na kifungu cha 84 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka hayo Oktoba 29, 2024, siku mbili baada ya kipande hicho cha video kuonekana katika mitandao ya kijamii akimshambulia mtu mwingine kwa mateke na kitako cha bastola na kuzuia mjadala.

Kesi ya jengo lililoanguka Kariakoo

Hii ni kesi iliyotokana na tukio la kuanguka kwa jengo la ghorofa lililoanguka Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo na kusababisha Vigo vya watu 31.

Novemba 29, 2024 wamiliki wa jengo hilo walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia, kinyume cha vifungu vya 195 na 198 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC).

Wamiliki hao wa jengo hilo ambao ndio washtakiwa katika kesi hiyo ni Leondela Mdete(49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam(61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.

Wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, washtakiwa hao isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya Said Juma na wenzake 30.

Kesi hiyo namba 33633/2024, itatajwa Januari 13, 2025 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Kesi ya jaribio la kumteka Tarimo

Hii ni kesi ya jinai inayotokana na tukio la jaribio la kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo, lililosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Picha za CCTV zikionyesha Deogratius Tarimo akichukuliwa kwa nguvu na watu watatu kutoka hotelini.

Katika tukio hilo lililotokea Novemba 11, 2024, video hiyo iliwaonesha watu wawili wakimvuta mtu mmoja mpaka kwenye gari lao, kisha wakijaribu kumbeba kumuingiza ndani ya gari hilo.

Hata hivyo, walipata upinzani mkali kutoka kwa mtu huyo aliyekuwa akipaza sauti za kuomba msaada akilalama kuwa anatekwa, jambo lililowafanya watekaji hao kumuachia na kuingia kwenye gari lao na kuondoka kwa kasi.

Related Posts