Jeshi la Magereza Tanzania Bara limemuonya Ofisa Habari wa zamani wa Yanga, Haji Manara dhidi ya kauli isiyokuwa ya kiungwana juu ya jeshi hilo anayodaiwa kuitoa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya timu hiyo na Tanzania Prisons uliochezwa juzi katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Yanga ilishinda kwa mabao 4-0, lakini baada ya kumalizika Manara anadaiwa kutoa maneno yasiyokuwa ya kiungwana shidi ya jeshi hilo.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo, Desemba 23, 2024 na Msemaji wa jeshi hilo, Kamishna Mwandamizi (SACP), Elizabeth Mbezi, imesema jana Jumapili Desemba 22, 2024 muda mfupi baada ya kumalizika mchezo Manara alionekana akibishana na watu wa Magereza waliokuwa wakimuomba asogeze gari lake ili wapitishe la kwao kwani alikuwa ameziba njia.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa: “Jeshi la Magereza Tanzania Bara linapenda kuujulisha umma kuwa limesikitishwa na kauli isiyo ya kiungwana iliyotolewa na Haji Sunday Manara baada ya kumalizika kwa mchezo Na 110, mzunguko wa 14 uliochezwa jana kati ya Young Africans na Tanzania Prisons katika Uwanja wa KMC Complex.
“Baada ya kumalizika kwa mchezo huo Haji Manara alianza kuongea na vyombo vya habari akiwa ameegesha gari lake mbele ya gari la Jeshi la Magereza. Kwa kuwa alikuwa amezuia gari la jeshi kuondoka aliombwa atoe nafasi kwa kusogeza gari lake kuruhusu gari alilokuwa amelizuia liweze kupita na yeye aendelee na mahojiano yake.
“Hata hivyo, pamoja na kuombwa alikataa kwa dharau na kuanza kutoa maneno yasiyo ya kiungwana, yenye viashiria vya kutweza utu na yenye mwelekeo wa kulifedhehesha Jeshi la Magereza.
“Uongozi wa Jeshi unatoa onyo na kuwataka wananchi kuacha kutoa kauli zenye mwelekeo wa kubeza, kutweza, kudharau mamlaka yake au kulifedhehesha na kwamba halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayehusika.”