Arusha. Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema anatarajiwa kuongoza hafla za makabidhiano na utambulisho wa viongozi wapya wa kanda hiyo kupitia mikutano ya hadhara itakayofanyika katika mikoa yote minne.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Desemba 23, 2024, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, amesema maandalizi yanaendelea na baada ya Lema kurejea kutoka Canada, ataongoza shughuli za makabidhiano pamoja na mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuwatambulisha viongozi wapya wa kanda hiyo.
“Tunamsubiri Lema ambaye kwa sasa yuko nchini Canada, atakaporejea tutafanya makabidhiano rasmi ya ofisi sambamba na mikutano ya hadhara katika mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini,” amesema Golugwa.
Amesema mikutano hiyo itafanyika katika miji ya Babati, Arusha, Moshi na Tanga, huku akieleza kuwa wanatarajia Lema atahudhuria mikutano yote hiyo.
Desemba 19, 2024, Chadema Kanda ya Kaskazini ilifanya uchaguzi na Samwel Welwel alichaguliwa kuwa mwenyekiti, huku Gervas Sulle kuwa makamu mwenyekiti na Emma Kimambo kuwa Mweka Hazina.
Uchaguzi huo ulifanyika jijini Arusha chini ya usimamizi wa mjumbe wa kamati kuu, Patrick Ole Sosopi.
Hivi karibuni, Lema alitangaza kutowania nafasi yoyote ya uongozi katika ngazi ya kanda na hakuhudhuria uchaguzi huo kutokana na kuwa na safari kuelekea Canada ilipo familia yake.