Maagizo manne ya Waziri Chana akimwapisha Kamishna wa NCAA

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana ametoa maagizo manne kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wakati akimwapisha na kumvisha cheo, Kamishna wa mamlaka hiyo, Dk Elirehema Doriye.

Katika maagizo yake aliyoyatoa leo Jumatatu, Desemba 23, 2024, Waziri Chana amesisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuimarisha utendaji, kuongeza weledi katika utangazaji, uhifadhi na usimamizi wa rasilimali fedha kwa manufaa ya Taifa.

Aidha, amesisitiza usimamizi wa haki za watumishi wanaosaidia utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, ikiwemo kuhakikisha wanapatiwa stahiki zao kwa wakati sambamba na kuwapeleka kupata mafunzo ya mara kwa mara yanatolewa ndani na nje ya nchi.

Hafla hiyo imefanyika wilayani Karatu, mkoani Arusha, yalipo makao makuu ya NCAA. Dk Doriye aliteuliwa Mei 7, 2024, kuchukua nafasi ya Richard Kiiza.

Katika maagizo mengine, Waziri Chana ametaka NCAA kuboresha na kuimarisha miundombinu ya barabara, madaraja na malango ili kuvutia watalii zaidi.

“Nataka pia muongeze juhudi katika uhamasishaji wa watalii wa ndani, ili kuongeza idadi yao wanaotembelea vivutio vilivyopo ndani ya Bonde la Ngorongoro,” amesema.

Amesema kati ya Julai na Novemba mwaka huu, zaidi ya watalii 550,000 kutoka mataifa mbalimbali wametembelea Ngorongoro, huku watalii wa ndani wakiwa 201,000 pekee.

Hivyo, Waziri huyo amesisitiza haja ya kuongeza kampeni za ndani, ili kuvutia Watanzania wengi zaidi kutembelea vivutio vya hifadhi hiyo.

Amesema utekelezaji wa maagizo hayo utasaidia kufanikisha lengo la Serikali la kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola bilioni sita (zaidi ya Sh15 trilioni 15) ifikapo mwaka 2025.

Aidha, amuelekeza Kamishna, Dk Doriye kuhakikisha utekelezaji wa majukumu aliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan, hasa katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Ngorongoro pamoja na kutangaza vivutio vya malikale vilivyopo katika hifadhi hiyo.

Kwa upande wake, Kamishna Dk Doriye ameahidi kusimamia uhifadhi endelevu kwa maslahi ya Taifa na vizazi vijavyo, kuhamasisha matumizi ya teknolojia, kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuimarisha miundombinu ya hifadhi hiyo.

“Uhifadhi endelevu unategemea utunzaji wetu. Nitaakikisha usemi wa ‘tumerithishwa, tuwarithishe’ unatekelezwa kwa vizazi vijavyo,” amesema kamishna huyo.

Amesema wataongeza ushirikiano na jamii zilizoko ndani ya mamlaka katika mipango ya uhifadhi wa wanyamapori, misitu na malikale, pamoja na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA, Jenerali mstaafu Venance Mabeyo amesema wana imani kubwa na uongozi wa Kamishna Dk Doriye na kuahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pia amemtaka kamishna huyo kusimamia kwa umakini masuala makuu matatu ambayo ni uhifadhi endelevu, kuendeleza utalii na maendeleo ya jamii.

“Tunategemea uongozi wako, maono yako, uvumilivu wako, na uzalendo wako katika kusimamia haya. Sisi kama bodi tuko tayari kushirikiana nawe kuhakikisha haya yanatekelezwa kwa ufanisi,” amesema Mabeyo.

Related Posts