Maaskofu waonya matukio ya utekaji, rushwa mwaka 2025

Moshi/Dar. Maaskofu wa madhehebu manne tofauti, wameibuka na mambo mbalimbali katika salamu zao za Krismasi 2024,  huku wakiweka msimamo wa kutaka kukoma kwa vitendo vya utekaji, kupotea kwa watu  na mauaji.

Katika salamu zao hizo walizotuma kwa waumini na Mwananchi kupata nakala, maaskofu hao ambao ni pamoja na Dk Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wametaka hatua zichukuliwe haraka.

Mwingine ni Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Method Kilaini,  aliyetoa  wito wa kuwekezwa nguvu ya udhibiti wa matukio ya utekaji, mauaji ya watu na vitendo vya rushwa ili yasitokee mwaka mpya 2025.

Wito kama huo, umetolewa pia na maaskofu wengine wengine wa madhehebu matatu  wakitaja mambo kadhaa, yakiwamo masuala ya utekaji, mauaji na demokrasia.

Msimamo wa viongozi hao, umekuja katika kipindi ambacho imesalia takriban wiki moja na ushei kabla ya  kumaliza mwaka 2024 na kuuanza mwaka mpya wa 2025.

Katika ujumbe wake, kuelekea Sikukuu ya Krismas itakayosherehekewa duniani kote Desemba 25, Askofu Kilaini amesema unapoingia mwaka 2025,  ni vema watu waombe msamaha na kumshukuru Mungu.

Kwa mujibu wa askofu huyo, msamaha huo unapaswa uombwe hasa katika maeneo yaliyoharibiwa akitolea mfano matukio ya watu kutekwa, kuuawa, wizi, unyang’anyi na rushwa.

“Kuna watu walitekwa, waliuawa, wizi na unyanganyi, rushwa, ajali ambazo zinaweza kuepukika. Familia ambazo zimefarakana kwa yote haya siyo tu tuombe msamaha,  bali tuweke nguvu mwaka ujao yasitokee tena na panapowezekana tuponye majeraha,” amesema.

Kwa kuwa mwaka 2025 kutakuwa na Uchaguzi Mkuu, amesema ni vema kumuomba Mungu uwe wenye amani, utulivu na haki utakaoleta mshikamano wa Taifa badala ya mafarakano.

“Mungu Mwenyezi awabariki na kuwaneemesha, awajaze fanaka na furaha yenye utauwa na uongofu na awalinde katika mwaka mpya wa 2025,” ameandika katika ujumbe huo.

Sambamba na hayo, Askofu Kilaini amesema Krismas ndiyo siku ambayo waumini wa dini ya kikristu wanakumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kadhalika ni siku yenye matashi mema kwa kila mwenye mapenzi mema.

Pamoja na kuwatakia heri ya siku hiyo Watanzania, askofu huyo amewasihi kuwa na upendo, ustahimilivu, mshikamano, heshima na kujaliana.

“Tuwe na amani moyoni mwetu, katika familia zetu na Taifa letu iliyojikita katika heshima na haki,” ameandika katika ujumbe huo.

Ameambatanisha maombi katika ujumbe wake huo, akiandika pale ambapo mtu alifanya vibaya mwaka 2024 aongoke na kuwa mpya na alipofanya vizuri aweke nguvu zaidi.

“Tumshukuru Mungu kwa mema mengi tuliyoyapata, uhai, afya, amani na maendeleo katika nchi yetu. Kuna mengi sana ya kutoa shukrani na kupongezana,” amesema.

Walichokisema Askofu Mbilu, Bagonza

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya KKKT, Dk Msafiri Mbilu amewataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kusherehekea sikukuu ya Krismasi mwaka huu kwa kutubu dhambi na kuacha yale yote ambayo hayampendezi Mungu.

“Tusherehekee Krismasi kwa kufanya matendo ya huruma tukiwasaidia wasiojiweza katika maeneo yetu mfano watoto yatima, wajane, wagonjwa na wafungwa,”amesema Askofu Mbilu katika salamu hizo na kuongeza:

“Tusherehekee Krismasi kwa kupinga na kukemea maovu ya kila aina katika jamii kama vile ukatili wa kijinsia, mauaji, watu kutekwa, wizi na ujambazi.”

Askofu Mbilu amewataka waendeshaji wa vyombo vya moto kama pikipiki na magari, watii sheria na kanuni za usalama barabarani, ili kuepusha ajali zinazopoteza maisha ya watu wengi, hivyo kupunguza nguvu kazi ya Taifa na jamii.

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Benson Bagonza,  amezungumzia masuala matano ya kijamii likiwamo la utekaji na watu kupotea.

“Habari za masikini kutajirisha matajiri si ngeni kwetu. Tumewaona wakulima masikini wakitajirisha matajiri, waumini masikini wakitajirisha wahubiri, Bodaboda masikini wakiwatajirisha wauza pikipiki na askari barabarani,” amesema askofu huyo.

Bagonza ameenda mbali na kueleza kuwa habari za wapiga kura masikini kutengeneza viongozi matajiri,  si ngeni pia miongoni mwa jamii ya Watanzania.

“Wakati huohuo hatuwaoni matajiri wanaowatajirisha masikini. Tunachokiona ni matajiri wanaodhani wana bidii na akili, masikini wanaoambiwa ni wavivu na hawana akili. Kwao hawa matajiri, kutajirika ni akili na ujanja.”

“Hawa matajiri huwaona masikini kuwa ni wavivu na wasio na akili, lakini ukweli ni kwamba utajiri na umasikini vina uhusiano wa karibu sana na mara nyingi uhusiano huu umejengwa katika unyonyaji.

“Kuzaliwa kwa Yesu kulileta picha tofauti. Yeye alikuwa tajiri ili masikini wawe matajiri na alizaliwa katika hali ya masikini ili sisi tuwe matajiri. Masikini na matajiri wote wana nafasi katika kuzaliwa kwa Yesu Kristo,”amesema Askofu Bagonza.

Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Askofu John Olotu katika salamu zake, ameitaka jamii itambue kuwa Mungu anawawazia yaliyo mema kila wakati hivyo nao wawazie mema watu wote.

“Tuache vitendo vya unyanyasaji, dhuluma, chuki na uadui maana sisi sote tu waja wake Mungu na kwake tutarejea na kila mtu atakwenda kusimama mbele ya kiti cha hukumu kutoa hesabu ya kazi zake alizofanya wakati akiwa hapa duniani,” amesema.

Akizungumzia mambo ya mauaji, watu kupotea na kuuawa, Askofu Olotu amesema yanaumiza mioyo ya Watanzania wengi.

“Hebu tufikiri kwa makini, kama ni ndugu yako ametoweka au ameuawa utajisikiaje mpendwa je, kama ni baba ametoweka watoto wake au mke wake wanasikia uchungu wa namna gani, jaribu kuvaa viatu vyao ujisikie itakuwaje,” amesema.

Ameongeza: “Lakini tujue kuwa damu inayomwagika pasipo hatia inadai kila mara, tujifunze kwa Kaini ambapo Bwana alimwambia Kaini damu ya ndugu yako inanililia kutoka ardhini.’’

Hata hivyo, amewaomba viongozi wote wa dini wasiache kumwomba Mungu ili ainusuru nchi na majanga hayo na waombe pia kwa ajili ya viongozi wa nchi hususan Rais Samia Suluhu Hassan na safu yake yote.

Ujumbe wa Askofu Mwamakula

Ujumbe wa Askofu Emmaus Mwamakula ulilenga katika mambo makuu sita ambayo ni pamoja na utekaji, kupotea na mauaji ya raia wasio na hatia, tatizo la ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama za maisha na gharama kubwa za matibabu.

“Tunaingia katika kusherehekea Krismasi wakati watu wetu wengi wapo katika hali ya mashaka, hofu hata kukata tamaa kwa mambo mengi sana,” amesema askofu huyo.

Amedai hali ya usalama kwa maisha ya watu na mali zao umezorota kwa kiasi kikubwa, vitendo vya utekaji na mauaji vimeiweka jamii ya Watanzania katika taharuki ambapo watu  kadhaa wameuawa na watu wasiojulikana.

“Vijana wetu kadhaa waliotekwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita hawajulikani waliko. Pia, hali ya usalama wa majengo nchini inaogopesha, moto unaunguza majengo huku mengine yakiporomoka na uwezo wa uokozi ni mdogo sana.”

“Bidhaa bandia zinatishia hali ya afya huku kukiwa na hofu ya uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wake madukani,”amedai Askofu Mwamakula.

Amesema ukosefu wa ajira nchini limekuwa janga linalotishia ustawi wa vijana. “Vijana wetu wengi waliohitimu katika shule, vyuo na vyuo vikuu wamejiingiza katika uhalifu wa aina mbalimbali kwa kukosa ajira ikiwemo wa mtandao.”

Amesema hata gharama za maisha nazo zimepanda juu kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa, huku kipato kikiwa hakijaongezeka na  gharama za matibabu katika baadhi ya hospitali nazo zikiwa juu na wananchi wengi hawawezi kuzimudu.

Askofu Mwamamkula katika ujumbe wake, amezungumzia pia hali ya ubora wa elimu kwa shule za Serikali,  akisema hauridhishi na kutaka juhudi ziongezwe ili kuzifanya ziwe bora zaidi.

Related Posts