-MAJIKO YA GESI 3,255 KUSAMBAZWA KWA BEI YA RUZUKU MAGU.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahakikishia wananchi wa Kijiji cha Ijinga kilichopo kwenye Kisiwa Wilayani Magu Mkoani Mwanza kijiji pekee kilichosalia kufikishiwa umeme wilayani humo kitafikiwa na kwamba zaidi ya shilingi milioni 600 imetengwa na Mkandarasi yupo eneo la mradi.
Amesema hayo Wilayani Magu Desemba 23,2024 wakati akihutubia wananchi katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Magu.
“Mnavijiji 82, vijiji 81 vyote vina umeme kimebaki kijiji kimoja kipo kwenye kisiwa na tuliona itachukua muda kuwapelekea umeme kwa kulaza nyaya kwenye maji tukaona watu wa Ijinga ni Watanzania wanastahili kupata umeme tumetenga milioni 619 ili nao wapate umeme,” alisema
Mhe. Biteko Alisema Mkandarasi yupo eneo la mradi Kampuni ya Master Volt Ltd yupo kwa ajili ya kupeleka umeme Jua (Solar).
Kwa upande wake Mbunge wa Magu, Mhe. Boniventura Kiswaga alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha umeme katika vijiji 81 kati ya vijiji 82 jimboni humo.
“Kazi kubwa imefanyika, umeme sasa 99%, tumebakiza kijiji kimoja tu cha Ijinga kwani vijiji 81 tayari vyote vina umeme,” alisema.
Aidha alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuibeba ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo alisema inakwenda kuokoa mazingira na afya zao.
“Naipongeza REA kwa kuibeba ajenda hii ya Mhe. Rais kwa kuandaa programu mbalimbali ikiwemo ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya 50%,” alisema Mhe. Kiswaga.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini, Msimamizi wa Miradi Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Awesa Rashid alisema REA inatekeleza miradi mbalimbali mkoani humo na kwamba baada ya kukamilisha kusambaza umeme vijijini na sasa ni zamu ya vitongoji.
“Tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 15 kwa kila Jimbo ikiwemo Jimbo la Magu ambapo kwa sasa mradi huu unaendelea,” alifafanua Mhandisi Awesa.
Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya shilingi 27,000 tu ili kujiletea maendeleo.
Aidha, akizungumzia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034, Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Ramadhani Mganga alisema REA inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa za nishati safi za kupikia ili kuepukana na adha mbalimbali zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi.
“Tumuunge mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034,” alisema Mhandisi Mganga.
Mhandisi Mganga alisema kwa upande wa Mkoa wa Mwanza jumla ya majiko 19,530 yatasambazwa ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50%.
“Tupo hapa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi. Napenda kuwahimiza wananchi wanapokwenda kununua mtungi huu wa ruzuku ni lazima uwe na kitambulisho cha Taifa,” alisisitiza.
Kwa nyakati tofauti wananchi waliipongeza Serikali kupitia REA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika suala zima la matumizi ya nishati safi.
“Mpango huu wa Serikali tumeupokea vizuri. Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ameturahisishia sisi watanzania tulikuwa tunakata miti ovyo ili kupata kuni na mkaa na sasa madhara yake tunayaona,” alisema Sebastian Boniphace Mkazi wa Magu.