Mshtakiwa aomba kesi ya uhujumu uchumi ifutwe, akidai upelelezi kuchelewa

Musoma. Mshtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kuifuta kesi hiyo kwa madai muda wa upelelezi kwa mujibu wa sheria umepita.

Mshtakiwa huyo, Gerold Mgendigendi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 kabla ya kesi hiyo kuahirishwa, baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi wake haujakamilika.

Katika kesi hiyo namba 22036/2024, Mgendigendi, aliyekuwa mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bunda na  Padri Carol Mwibule wa kanisa hilo Jimbo la Bunda, wanashtakiwa kwa makosa 178, ikiwemo la uhujumu uchumi.

“Ni zaidi ya siku 90 sasa tangu polisi waseme upelelezi umekamilika, lakini hadi sasa kila tukija hapa tunaambiwa upelelezi bado. Tunaomba kesi hii ifutwe, kwani kwa mujibu wa sheria upelelezi huwa unafanyika ndani ya siku 90 sisi huu wa kwetu umevuka muda huo,” amedai Mgendigendi.

Amedai hapakuwa na sababu ya wao kupelekwa mahakamani kama upelelezi haujakamilika, hivyo ni vema kesi hiyo ikafutwa na wao wakaachiwa huru.

Alijibu hoja kuhusu upelelezi kuchukua muda mrefu, Wakili wa Serikali, Agma Haule amedai kesi hiyo imefikishwa mahakamani Agosti mwaka huu na sio muda mrefu kama inavyodaiwa na mshtakiwa.

Hata hivyo,  mshtakiwa huyo alifafanua akidai kuwa polisi walianza upelelezi wa kesi yao takriban miaka miwili sasa.

Awali, Haule alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kumuomba hakimu kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Akiahirisha kesi hiyo leo, Hakimu Mkazi Mkuu, Eugenia Rujwahuka amesema itatajwa Januari 6, 2025.

Hakimu Rujwahuka amesema hana uamuzi juu ya hoja hiyo kwa kuwa kesi hiyo ipo kwa hakimu mwingine ambaye kwa sasa yuko likizo.

“Hoja yenu iko sawa, ila kwa leo tunaiahirisha kesi hii hadi tarehe tajwa ambapo itakuja kwa hakimu wenu mheshimiwa Mugendi ambaye kwa sasa yupo likizo, akija atatoa uamuzi,” amesema.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanashtakiwa kwa wizi wa fedha zaidi ya Sh1.7 bilioni pamoja na fedha za kigeni ikiwepo Dola zaidi ya 100,000  na Euro zaidi ya 20,000.

Washtakiwa wanakabiliwa na makosa 178, likiwemo kosa la kuongoza genge la uhalifu, kinyume na sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022 na makosa mengine ni utakatishaji wa fedha kinyume na sheria ya adhabu sura ya 16.

Related Posts