Mwanafunzi Udom afariki dunia mafunzoni Udzungwa

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza taarifa ya kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Hezekiel Petro (21) aliyekufa maji kwenye maporomoko ya maji Sanje yaliyopo Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Kata ya Sanje, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea jana Jumapili, Desemba 22, 2024.

Kamanda Mkama amesema Hezekiel, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho akisomea masomo ya sanaa na historia, alikufa maji baada ya kukanyaga jiwe lenye utelezi na kutumbukia kwenye maji yenye kina kirefu.

“Tunachunguza tukio la Hezekiel Petrol, aliyefikwa na mauti baada ya kukanyaga jiwe lenye utelezi na kutumbukia katika maji yenye kina kirefu na kupoteza maisha wakati alipotembelea Hifadhi ya Idzungwa na wanafunzi wenzake kwenye ziara ya mafunzo kwa vitendo,” amesema Kamanda Mkama.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Alex Mkama

Kamanda Mkama amesema wanafunzi zaidi ya 300 wakiwa wameambatana na wakufunzi wao walikuwa kwenye ziara ya mafunzo kwa vitendo eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya wataalamu wanapotembelea maeneo yenye upekee.

Related Posts