RAIS DKT SAMIA AWATAKA WANANCHI KUFANYA MAZOEZI KULINDA AFYA ZAO.

Na WILLIUM PAUL, ROMBO.

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Rombo mkoani Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla kuendelea kufanya mazoezi kwa wingi ili kulinda afya zao.

Hayo yamebainishwa leo na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa Tamasha la mbio fupi la Rombo marathon and Ndafu festival lililofanyika katika viwanja vya Rongai wilaya Rombo.

Dkt. Kikwete alisema kuwa, wakati anampa taarifa za kuja Rombo kuwa mgeni rasmi katika Tamasha hilo kwa njia ya simu alimwandikia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na kumtaka kuwafikishia ujumbe huo wananchi watakaokuwa wameshiriki Tamasha hilo.

“Naomba nisome ujumbe wa Rais Dkt Samia alisema niwasomee ‘Jambo hilo la Rombo marathon linakubalika sana waeleze kabisa wananchi na niwahimize wananchi wa Rombo na Watanzania kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga afya zao” Ujumbe mfupi wa Rais Dkt. Samia ulisomeka hivo.

Na kuongezea “kwa kutambua umuhimu wake nimemtuma mshauri wangu wa maswala ya Afya Profesa Muhammed Janadi aje huko kutoka ofisini kwangu”.

Dkt. Kikwete alisema kuwa, ameridhishwa na lengo la Tamasha hilo ambapo fedha zinazopatikana hupelekwa kuboresha miundombinu ya hospitali ya Huruma ili iweze kutoa huduma ngazi ya mkoa pamoja na fedha nyingine kupelekwa kukabiliana na changamoto ya matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

“Baada ya kuambiwa malengo ya Rombo marathon niliridhika nayo na kunishawishi leo hii nije kuwa mgeni rasmi kwani fedha zinazopatikana zinarudi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Rombo na Watanzania kwa ujumla” Alisema Dkt. Kikwete.

Alisema kuwa, Rombo ya sasa sio ile ya mwaka 2005 kwani imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo kwani zipo barabara za lami lakini pia ipo miradi mikubwa ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika wilaya hiyo.

Rais huyo Mstaafu alisema kuwa, anatambua kazi badi haijafika mwisho kwani hawajafika pale walipokusudia kufika na kuwataka wananchi kuendelea kuwaunga mkono viongozi wao na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha inaendelea kusonga mbele kwa kupiga hatua.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Rombo na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa, Tamasha hilo la Rombo marathon limekuwa likikuwa mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka huu ni awamu ya tatu ambapo limekuwa likiwakutanisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi.

 

Related Posts