Serikali kuanzisha uchunguzi baada ya shambulio la Magdeburg – DW – 23.12.2024

 

Mwanamume anayeshukiwa kulivurumisha gari lake katikati ya umati wa watu waliokuwa kwenye soko la Krismasi katika mji wa Magdeburg ulio Katikati mwa Ujerumani tayari amefikishwa mahakamani na anakabiliwa na mashtaka ya mauaji na kujaribu kuua, hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Soma Zaidi: Ujerumani yachunguza maonyo kuhusu muuaji wa soko la Krismas

Mshukiwa, Taleb A. ambaye alikuwa kizuizini, ni daktari wa maradhi ya akili mwenye umri wa miaka 50 mwenye asili ya Saudi Arabia, ni mtu mwenye historia ya kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu ambaye ameishi nchini Ujerumani kwa takriban miongo miwili.

Sababu ya yeye kufanya mashambulio hayo ya siku ya Ijumaa (Desemba 20) jioni bado haijafahamika.

Magdeburg | Soko la Krismasi
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alipozuru soko la Krismasi la Magdeburg baada ya shambulioPicha: Marc Erath/DW

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ameahidi kwamba serikali yake itajibu tukio hilo baya kwa nguvu kamili ya sheria lakini pia ametoa wito wa kuwa na umoja. Ujerumani sasa imekumbwa na mjadala mkali kuhusu uhamiaji na usalama kabla ya uchaguzi wa mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari.

Mgogoro wa kisiasa umeibuka nchini Ujerumani baada ya shambulio kwenye soko la Krismasi huko Magdeburg na umeibua maswali mengi kuhusu hali ya usalama na udhaifu katika idara za kijasusi nchini Ujerumani.  Wakati huo huo chama cha mrengo wa kulia kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani AfD kimepanga kufanya mikutano na maandamano ya maombolezo siku ya Jumatatu katika mji wa Domplatz wa mashariki mwa Ujerumani  siku ya Jumatatu.

Mgombea wa ukansela wa chama hicho katika uchaguzi wa mwezi Februari, Alice Weidel na wanasiasa kadhaa wa chama cha AfD wanatarajiwa kuhudhuria.

Ujerumani | Magdeburg | Waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Faeser
Katikati: Waziri wa mambo ya Ndani wa Ujerumani NancyFaeser alipozuru soko la Krismasi la MagdeburgPicha: Ebrahim Noorozi/AP/picture alliance

Tukio sambamba kama hilo limeandaliwa na kundi linalopinga chuki, kundi hilo na wafuasi wao kwa kulizunguuka soko la Krismasi la Magdeburg ambako mhalifu Taleb A. aliwashambulia watu mwishoni mwa wiki iliyopita. Kati ya watu watano waliouawa alikuwemo mtoto wa miaka 9. 

Soma Zaidi: Magdeburg: Maswali yaibuka kuhusu hali ya usalama Ujerumani

Wakati huo huo polisi katika mji wa bandari wa Bremerhaven, wamemkamata mtu mmoja baada ya mtu huyo kuchapisha video yake kwenye mtandao wa Tik Tok, akitishia kuwa atafanya mashambulio mabaya zaidi katika soko la Krismasi kwenye mji huo.

Vyanzo: DPA/AFP

 

Related Posts