Dar es Salaam. Serikali imeajiri mshauri wa kufanya tathmini ya Gridi ya Taifa kushughulikia changamoto za kimfumo zinazotokea na kusababisha mgawo wa umeme nchini na nchi jirani.
Tanzania imekuwa ikikumbwa na mgawo wa umeme, unaosababisha usumbufu kwa huduma za treni za umeme (SGR) kutokana na changamoto zilizopo katika Gridi ya Taifa.
Matukio yalitokea wiki iliyopita baada ya hitilafu ya kiufundi katika Gridi ya Taifa yalisababisha mgawo wa umeme nchini Kenya, ikiwa ni siku chache baada ya kuanza kwa biashara ya umeme kati ya nchi hizo.
Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Styden Rwabangila, ameliambia gazeti dada la The Citizen kwamba timu ya wataalamu kwa sasa inachunguza changamoto zilizopo katika gridi ili kuja na suluhisho.
“Kwa kawaida, gridi ina mfumo wa kinga ambao huzuia athari za kusambaa kwa kiasi kikubwa pale changamoto zinazojitokeza,” ameeleza.
Ametaja tukio la hivi karibuni katika eneo la Victoria, ambapo upepo mkali ulidondosha bango kubwa kwenye nyaya za umeme, kuathiri gridi nzima.
Rwabangila amethibitisha kwamba mshauri ameshaanza kazi na anatarajiwa kumaliza ripoti ya kina ndani ya miezi mitano, akipendekeza hatua za kurekebisha, ili kuboresha uimara wa gridi.
Wakati wa ukaguzi wa hivi karibuni katika kituo cha umeme Kinyerezi, Novemba 18, 2024, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alisisitiza uboreshaji wa miundombinu ya umeme unaendelea katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema kuwa maboresho hayo, ikiwemo ufungaji wa transfoma mbili za 75 MVA, yataongeza uwezo wa kituo hicho kufikia 180 MVA, na kuhakikisha kuna umeme wa kutosha katika maeneo kama Gongo la Mboto, Mbagala na Kigamboni.
“Maboresho haya yataondoa upungufu na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme katika jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Pwani,” alisema.
Kapinga alielezea pia miradi mingine, ikiwemo ujenzi wa kituo cha umeme cha Mabibo na maboresho ya njia ya umeme ya Kibaha-Ubungo na Ununio-Ubungo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Gissima Nyamo-Hanga, alibainisha kuwa mahitaji ya umeme katika jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Pwani yameongezeka kwa asilimia 16, na kufikia megawati 738. Ongezeko hilo limelazimu maboresho hayo, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Hivi karibuni Nyamo-Hanga alielezea ushiriki wa Tanzania katika mradi wa East Africa Power Pool (EAPP), jitihada za ushirikiano zinazohusisha nchi 13 zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa hadi megawati 90,000.
“Ushirikiano huu unarahisisha biashara ya nishati, ambapo nchi zenye ziada ya umeme zinauza kwa zile zenye upungufu, hivyo kukuza ushirikiano wa nishati katika kanda,” alifafanua.
Nyamo-Hanga alielezea kuhusu kukamilika kwa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Lemuguru cha 400kV. Alisema kuwa Tanzania na Kenya sasa zimeunganisha gridi zao za umeme kupitia kituo hiki, ambacho ni muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kati ya nchi hizo na wanachama wengine wa EAPP.
“Kukamilika kwa kituo hiki ni hatua kubwa katika lengo la kuunganisha gridi za umeme za Tanzania na Kenya,” alisema.
Kituo cha Lemuguru kilichopo Arusha kinahusika na umeme wa voltage ya juu ya 400kV na ni muhimu katika kuunganisha gridi za umeme za Tanzania na Kenya. Mfumo huo wa gridi uliounganishwa unarahisisha uhamishaji na biashara ya umeme kati ya nchi hizo na mataifa mengine ya Mashariki na Kaskazini mwa Afrika.
Nyamo-Hanga pia alielezea kuwa Tanzania sasa imeunganishwa katika mfumo wa umeme wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ikiiweka nchi katika nafasi ya kipekee katika mitandao hii ya kanda, kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Hata hivyo, Septemba mwaka huu, Serikali ilisema kuwa haijafanya uamuzi wowote kuhusu kuagiza umeme kutoka Ethiopia, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kikanda na uwepo wa fursa ya biashara ya umeme kati ya nchi hizo.