Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewaagiza walimu kufundisha kwa kutumia ramani ya Tanzania inayoonyesha mpaka wa Ziwa Nyasa umepita katikati ya ziwa na siyo inayoonyesha kuwa ziwa lipo upande wa Malawi.
Maelekezo hayo yametolewa katika barua iliyosainiwa na Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk Lyabwene Mtahabwa ya Desemba 16, 2024 na kutumwa kwa wamiliki wa shule zisizo za serikali na kwa wadhibiti wakuu ubora wa shule na wilaya.
“Hakikisheni wanafunzi wote wanafundishwa hivyo na siyo kwa kutumia ramani ya geogle ambayo ina makosa,” amesema Dk Mtahabwa.
Amesema wizara hiyo ilipokea barua kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Novemba 26, 2024 kuhusu mgogoro wa Ziwa Nyasa na hatua zinazochukuliwa na Malawi kuhalalisha umiliki wa Ziwa Nyasa.
Dk Mtahabwa ameithibitishia Mwananchi leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 kuwa barua hiyo ni halisi, amesema ramani ya Tanzania inayopatikana katika tovuti ya google mpaka wake umebadilishwa na kuonyesha unaishia maji ya Ziwa Nyasa.
“Kwa sasa Malawi wanafundisha wanafunzi wao mabadiliko hayo ya ramani kuanzia elimu ya msingi na sekondari,” amesema.
Amesema kutokana na kukua kwa elimu na matumizi ya Tehama, kuna uwezekano mkubwa wa wanafunzi wa Kitanzania wanaotumia mitandao wakatumia ramani ambazo si sahihi kwa kujua au kutokujua mabadiliko yaliyopo kwenye ramani hizo.
“Kwa barua hii, wizara inaelekeza walimu wote wa shule zisizo za Serikali nchini wafundishe kwa kuzingatia mitalaa iliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Tanzania (TET),” amesema Dk Mtahabwa.
Benjamin Mkonya, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Vyuo na Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), amesema wanashukuru Serikali kwa barua hiyo ambayo inawarudisha kwenye uzalendo.
“Ni waraka mzuri na kama kuna waraka utakaokumbukwa na vizazi na vizazi ni huo … Lazima iingie kwenye akili za wanafunzi mipaka yetu iko wapi,” amesema.
Amesema waraka huo unafungua macho Watanzania katika mambo mbalimbali ambayo kama yasipoangaliwa na kuchukuliwa hatua miaka 20 ijayo inaweza kuharibiwa.
Amesema waraka huo unatakiwa kupanulia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo suala la watu kutoka nje wanaotaka kuimeza Tanzania kibaiolojia (kuzaa na Watanzania).
Mkonya amesema zipo baadhi ya nchi zimemezwa na nchi nyingine kwa sababu ziliweka mikakati ya kuzaa na watu wa nchi walizokuwa wakilenga kuzimeza na kufanikiwa.
“Tuendelee kushukuru huo waraka, lakini tuendee kuiomba Serikali kuangalia kwa macho mawili wageni wanaoingia nchini kwa malengo ya kuiteka nchi kwa kibaiolojia,” amesema.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema maelekezo hayo ni mazuri kwa sababu ni lazima watoto waandaliwe ili kujua jiografia ya nchi yao.
Hata hivyo, amesema mgogoro ni wa kihistoria ambao inabidi Serikali kukaa na watu wa kihistoria kwa ajili ya kuweka mkakati wa kuutatua.
Amesema wakoloni (Wajerumani na Waingereza) ambao waliitawala Tanzania waliweka mipaka ambayo wakati mwingine ilikuwa na maslahi yao.
“Kwa hiyo kinachotakiwa ni Serikali kujaribu kuutatua mgogoro kwa kutumia historia na diplomasia kwa sababu haiwezi kuishia hapo tu, hili sakata limekuwepo kwa muda mrefu sasa kiasi kwamba ni lazima litafutiwe suluhisho la kudumu,” amesema.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania ilitoa leseni kwa kampuni za kigeni kutafuta mafuta katika eneo hilo la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Chanzo cha mgogoro huo kimetokana na mikataba yenye utata iliyoachwa na wakoloni.
Kwa kulitambua marais waliotangulia hasa Bakili Muluzi na Bingu wa Mutharika wa Malawi na wenzao Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wa Tanzania waliendelea na mazungumzo.
Baada ya Rais Banda kuingia madarakani mgogoro huo ulizidi, hasa baada ya kubainika kuwa katika ziwa hilo kuna kiasi kikubwa cha mafuta.