Shaban Chilunda aingia anga za KMC

UONGOZI wa KMC uko katika mazungumzo ya kupata saini ya aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Shaaban Idd Chilunda baada ya kocha Kally Ongala kutoridhishwa na eneo hilo katika michezo 15 ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.

Chilunda aliwahi kuichezea timu hiyo kwa mkopo Januari, mwaka huu akitokea Simba ambayo aliachana nayo Julai Mosi mwaka huu, hivyo kwa sasa ni mchezaji huru jambo ambalo linaufanya uongozi kuanza hesabu za kumpata moja kwa moja kikosini.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza nyota huyo wa zamani aliyewika na timu za Azam FC, CD Tenerife ya Hispania na Moghreb Atletico Tetouan ya Morocco, kwa sasa anaendelea kufanya mazoezi akiwa na kikosi hicho cha kwanza cha KMC.

“Tupo naye hapa lakini siwezi kusema wazi tumemsajili kwa sababu kuna taratibu bado hazijakamilika, kama itakuwa hivyo basi tutawaeleza mashabiki wetu kwani huu ndio muda wa maboresho ya timu na lolote linawezekana,” kilisema chanzo chetu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema hawezi kuzungumzia suala la mchezaji huyo ingawa kama viongozi walishaanza taratibu zote za kukamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji, kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.

“Tutasajili kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi ila nikuhakikishie sisi hatutafanya maboresho makubwa kwa sababu waliopo wengi wao tutaendelea nao pia, ni baadhi ya maeneo madogo tu ambayo tutayaboresha katika dirisha hili dogo,” alisema.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua Chilunda huenda akajiunga na kikosi hicho ambacho anafanya kwanza majaribio ili kwanza kumridhisha kocha, Kally Ongala.

 Ongala anahitaji kuboresho eneo la ushambuliaji ili kuwaongezea nguvu nyota waliopo ambao ni Daruweshi Saliboko ambaye hadi sasa amefunga mabao mawili tu, huku kikosi hicho kikifunga mabao 10 na kuruhusu 15 katika michezo 15 ya raundi ya kwanza.

Akiwa na Simba, Chilunda hakufunga bao lolote la Ligi Kuu Bara ingawa wakati akiichezea KMC alifunga moja katika mchezo ambao kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni kilitoka sare ya 1-1, dhidi ya maafande wa JKT Tanzania Februari 27, 2024.

Related Posts