Sita wafariki dunia kwa kuangukiwa na gema, kusombwa na mafuriko Same

Same. Watu sita wakiwemo wawili wa familia moja wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kupata maafa yaliyotokana na mvua wilayani humo.

Watu hao wamefariki kati ya Desemba 20 hadi 22, 2024 na wanne baada ya nyumba zao kuangukiwa na gema usiku wakiwa wamelala, huku wengine wawili wakisombwa na maji ya mafuriko.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Mkaguzi Msaidizi Jeremiah Mkomagi amesema matukio hayo yametokea usiku wa Desemba 20, 2024.

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Joyce Elifuraha (57) na mumewe Elifuraha Elienea (59), wakazi wa Kijiji cha Mjema pamoja na Hamu Ally (76), mkazi wa Kijiji cha Miombo kata ya Mtii, ambao walifariki baada ya nyumba zao kuangukiwa na gema usiku. Mke wa Hamu amejeruhiwa.

Wengine waliofariki ni Elibariki Fanuel (48), mkazi wa Kijiji cha Vuje, Lazaro Saikon (35), mkazi wa kijiji cha Mheza na Eliakunda Elisafi (69), mkazi wa Kijiji cha Duma.

“Kuanzia Desemba 20 hadi 22, tumepokea taarifa za vifo vya watu sita katika Wilaya ya Same na majeruhi wapo wanne, wanaume wawili na wanawake wawili ambao wanaendelea na matibabu Hospitali ya Gonja Lutheran na hali zao zinaendelea vizuri” amesema Mkomagi.

Aidha, amesema kwa tathmini waliyofanya katika Kata ya  Bombo, nyumba 24 zenye kaya 104  zimeathiriwa na maafa hayo na nyumba 18 zimeanguka kabisa na nyingine zikipata nyufa.

“Mbali na vifo wapo wananchi ambao nyumba zao zimeathirika katika Kata ya Bombo, kuna nyumba tano zenye jumla ya kaya 19 na nyumba nne zimeanguka kabisa.

“Katika Kijiji cha Mjema, nyumba 14 zenye kaya 66 zimepata maafa na 11 zimebomoka kabisa. Nyumba tatu zimepata nyufa na katika Kijiji cha Mvaa nyumba tano zenye kaya 19 zimepata maafa, huku tatu zikibomoka kabisa,” amesema.

Akizungumza tukio hilo, Diwani wa Bombo, Philemon Msuya amesema mvua iliyonyesha usiku wa Desemba 20 kuamkia  Desemba 21, 2024 imesababisha maafa makubwa ya vifo na uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Msuya amesema kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa ukanda wa mlimani, mvua hizo zimesababisha maporomoko ya mawe na magema kuangukia nyumba na kusababisha vifo vya watu wawili ambao ni wanandoa katika Kijiji cha Mjema na baadhi ya wananchi kukosa makazi.

“Mvua imeleta matatizo makubwa, kwanza imeharibu miundonbinu ya barabara, sasa hazipitiki. Familia nyingi zimepoteza makazi katika kata hii kwa nyumba kuanguka,” amesema.

“Mvua kubwa ilinyesha kwa muda mrefu usiku wa Desemba 20 na ndiyo ilisababisha gema kuangukia nyumba ya Elifuraha na kusababisha kifo chake na mkewe,” amesema.

Amesema hatua ambazo wamechukua kwa sasa ni pamoja na kuhamisha wananchi waliopo maeneo hatarishi na wamehifadhiwa kwa ndugu jamaa na marafiki waliopo maeneo salama.

“Pia tayari tumewasiliana na viongozi wa wilaya ili kuona namna ya kufanya ili kukarabati miundombinu ya barabara ili kurudisha mawasiliano katika kata hii ya Bombo,” amesema Msuya.

Related Posts