Dodoma. Wafanyabiashara katika Mkoa wa Dodoma wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuweka utaratibu wa kupatikana kwa namba ya malipo ufanywe kwa njia ya simu badala ya kupanga foleni ofisini.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, utaratibu wa sasa unaowalazimu kwenda kuilipia namba hiyo katika ofisi za mamlaka hiyo, unawapotezea muda.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Dodoma, Gilbert Chuwa alipozungumza na TRA kujadili changamoto zinazowakabili.
Amesema upatikanaji wa namba za malipo kwa sasa unawalazimu kuzifuata zilipo ofisi za TRA, hivyo wangetamani utengenezwe utaratibu wa kuzilipia na kuzipata kwa njia ya simu.
Mbali na hilo, ameisihi mamlaka hiyo kuhamasisha ulipaji wa kodi, huku ikiendelea na juhudi za kuwasaka walipakodi wapya ili kuongeza kiwango cha makusanyo.
“Kuna wafanyabiashara wengi wasiolipa kodi kwa sababu hawana elimu sahihi, nashauri TRA iendelee kutafuta walipakodi wapya ili kuongeza makusanyo ya Serikali kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi wa TRA, Onesmo France amewasihi wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari, ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema ulipaji wa kodi kwa hiari unasaidia nchi kutekeleza miradi ya kimkakati inayofanywa kwa fedha za ndani, ikiwemo ujenzi wa hospitali, barabara na huduma za maji.
“Tuendelee kuhamamsha wananchi kulipa kodi kwa hiari ili fedha zitakazopatikana zitasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kujenga Taifa lenye uchumi imara,” amesema.
Pia, amewataka maofisa wa TRA kuwa na uhusiano mzuri na walip kodi, pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu faida za kulipa kodi.
Meneja wa mamlaka hiyo mkoani Dodoma, Pendolake Elinisafi amesema hivi sasa wametenga siku ya Alhamisi maalumu kwa ajili ya kusikiliza kero za wafanyabiashara, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Kamishna Mkuu, Yusuph Mwenda.
“Tumeanzisha mpango maalumu wa kusikiliza kero zinazowakabili wafanyabiashara ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi na kuhakikisha kila mtu analipa kodi kwa hiari,” amesema.