Wanane mbaroni wakituhumiwa uvunjaji vibanda vya biashara

Musoma.  Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, linawashikilia watu wanane kwa tuhuma za kuvunja vibanda 15 vya maduka na kuiba mali ambazo thamani yake bado haijajulikana eneo la Kariakoo Manispaa ya Musoma.

Watu bao wanadaiwa kufanya tukio hilo usiku wa kuamkia Desemba 22, 2024 na baada ya kuvunja, walichukua vitu mbalimbali pamoja na fedha taslimu kutoka katika maduka hayo.

Taarifa ya kukamatwa kwa watu hao, imetolewa leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo alipozungumza na waandishi wa habari.

Amesema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na msako bado unaendelea kuhakikisha wengine wanaotuhumiwa kushiriki katika tukio hilo wanapatikana.

“Hawa watu naweza kusema ni vibaka kwani baada ya kuvunja walikuwa wanatafuta pesa taslimu lakini bahati nzuri kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara hawa hawaachi pesa madukani,  hivyo mbali na kuchukua kiasi kidogo cha pesa walichobahatisha kukikuta na vitu kadhaa pia waliamua kula viporo vya wali na nyama walizokuta kwenye baadhi ya maduka,” amesema Lutumo.

Hata hivyo, amesema jeshi hilo limefanikiwa kukomesha vitendo vya uvunjaji wa maduka mkoani humo kwani ni zaidi ya miezi sita hakuna matukio ya aina hiyo yaliyotokea.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika maeneo yao ya makazi na biashara, badala ya kutegemea ulinzi wa jeshi hilo.

“Sisi tunatoa ulinzi wa umma, hatuwezi kumlinda mtu mmoja mmoja, hivyo ni vema wale wenye maduka au biashara wakawa na walinzi katika maeneo yao hii itasaidia kuepuka matukio ya wizi katika biashara badala ya kutegemea ulinzi wa polisi unaofanywa kwa njia za doria, ulinzi ambao tunasema ni wa umma,” amesema.

Kamanda Lutumo ametoa wito huo baada ya kubaini kuwa eneo la Kariakoo lenye vibanda vya maduka zaidi ya 100 lilikuwa na mlinzi mmoja wakati tukio la uvunjaji wa maduka hayo likitokea.

Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, amesema kutokana na tukio hilo tayari wameunda kamati itakayoratibu namna ya kuweka ulinzi katika eneo hilo.

“Ni kweli tulikuwa na mlinzi mmoja tena ambaye kidogo umri wake ni mkubwa lakini jana tulikutana na kuunda kamati ambayo itakuja na mapendekezo juu ya ulinzi wa eneo letu kama ni kutafuta walinzi kutoka kwenye kampuni au walinzi binafsi,” amesema.

Related Posts