Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limewakamata watuhumiwa 81 katika oparesheni maalumu, huku mmoja akitoroka na kutelekeza silaha aina ya gobore katika Kijiji cha Bugomba “A”, Kata ya Ulewe, wilayani Ushetu.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 na kamanda wa polisi wa mkoa huo, Janeth Magomi, alipozungumza na waandishi wa habari akitoa muhtasari wa mafanikio ya jeshi hilo kuanzia Novemba 27, 2024 hadi Desemba 22, 2024.
“Watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi wakiwa na vielelezo mbalimbali, ikiwemo madini bandia gramu 250 yanayodhaniwa kuwa dhahabu, bangi gramu 9,000, mirungi bunda 9, pombe za moshi lita 113, sola paneli 7, betri za sola 4, pikipiki 11, kadi za pikipiki 3,” amesema.
Vitu vingine vilivyokamatwa ni antena za ving’amuzi 4, simu 3, redio 2, baiskeli 2, mashine ya bonanza 1, camera 1 na mitambo ya kutengeneza pombe za moshi 4.
Pia amesema mtu mmoja amekimbia na kutelekeza silaha aina ya gobore, baada ya kuona gari la Polisi likiwa katika doria katika Kijiji cha Bugomba ‘A’ Kata ya Ulewe Wilaya ya Ushetu.
Aidha, Magomi ameeleza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja jumla ya kesi 18 zilifunguliwa, zikiwamo kesi mbili za kubaka na washtakiwa wawili wamehukumiwa miaka 30 jela kila mmoja, kesi kesi ya unyang’anyi kwa kutumia silaha na kulawiti mwanamke na washtakiwa wanne wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Nyingine ni kesi ya kumiliki nyaraka za Serikali ambapo washtakiwa watatu wamehukumiwa jela miaka 17 na miezi mitano.
Kwa upande wa utoaji elimu, amesema jeshi hilo limefanya mikutano 97 na Desemba 6, 2024 lilizindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.