Watuhumiwa kesi ya uhujumu miundombinu ya SGR waongezewa shtaka

Kibaha. Watuhumiwa watano wakiwamo raia wawili wa China wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu wa miundombinu ya treni ya kisasa (SGR), wameongezewa shtaka moja jipya.

Shtaka lililoongezwa ni la utakatishaji fedha, ambalo halikuwepo kwenye hati ya mashtaka ya awali walipofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani kwa mara ya kwanza Desemba 17, 2024.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Zhang Feng, Wang Yong, Paulo John, Abdul Mohamed, na Pius Kitulya, wote wakazi wa Miwaleni, Mlandizi, Kibaha.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Daudi Basaya, mahakamani hapo leo Jumatatu, Desemba 23, 2024, wastakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Novemba na Desemba 2024.

“Watuhumiwa wameongezewa shtaka moja la utakatishaji fedha, na upelelezi bado unaendelea. Tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine,” amesema Basaya.

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Felister Ng’welu, amewaeleza watuhumiwa hao kuwa hawapaswi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Mwendesha mashtaka ameeleza upelelezi unaendelea na kuiomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa utetezi Nestory Wandiba, alieleza kuwa wateja wake wanne wamekubali kuandika barua ya kuomba shauri hilo lisikilizwe nje ya mahakama kwa njia ya maelewano.

“Leo wateja wangu wameongezewa shtaka la utakatishaji fedha ambalo halina dhamana, lakini wameamua kuandika barua ili shauri hili limalizwe kwa njia ya maelewano, nje ya mahakama,” amesema Wandiba.

Baada ya hoja hizo, mwendesha mashtaka ameeleza kuwa ombi hilo litajibiwa kesi hiyo itakapokuwa ikiendelea.

Watuhumiwa wamerudishwa rumande na kesi itatajwa Januari 6, 2025.

Related Posts