Mamlaka ya Mji Mkongwe Zanzibar imepiga marufuku upigaji wa makachu katika eneo la bustani ya Forodhani, baada ya kudaiwa kufanyika vitendo vinavyokiuka maadili.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo jana Jumapili, Desemba 22, 2024 imeeleza uamuzi huo umefikiwa baada ya kuona kuna ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozo yaliyojitokeza kwa vijana wa makachu katika eneo hilo.
Imetaja pia ukiukwaji huo inahusisha upigaji makachu kwa kutumia mavazi yanayokwenda kinyume na utamaduni, uharibifu wa mifereji na miundombinu mengine, ikiwa ni pamoja na kutumia madebe taka kufanyia vichekesho (comedy).
Aidha, mamlaka hiyo imesema imesimamisha shughuli hizo hadi kukamilika na kuandaa utaratibu wa kuimarisha utendaji kazi hizo, kwani Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na vijana hao katika kuutangaza Utalii wa Zanzibar kimataifa.
Vilevile, mamlaka hiyo imeeleza inafanya uchunguzi wa matukio hayo na kuwachukulia hatua wale wote waliobainika kutenda makosa hayo, ikiwemo uharibifu wa miundombinu.
Hivi karibuni ilisambaa video ikionyesha baadhi ya watu ambao ni wa raia wa kigeni wakipiga makachu eneo hilo wakiwa na nguo ambazo haziendani na maadili ya Zanzibar.